Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Kigamboni Mwapemba, Rehema Hassan (42) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la mauaji.
Rehema anadaiwa kumuua muongozaji na msimamizi wa sauti za filamu nchini, Athuman Nyanza.
Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake leo Jumatano, April 29, 2026 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wencelaus, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Mshtakiwa Rehema Hassan, akiwa ameziba uso, akisindikizwa na askari polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa shtaka la mauaji ya muongozaji wa filamu, Athuman Nyanza. Picha na Hadija Jumanne.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka lake, Hakimu Swallo alimueleza mshtakiwa huyo kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Pia, shtaka linalomkabili mshtakiwa halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo atapelekwa rumande hadi upelelezi utakapokamilika.
Hakimu Swallo baada ya kutoa maelezo hayo, upande wa jamhuri walimsomea shtaka lake.
Mshtakiwa Rehema Hassan, akiwa ameziba uso, akisindikizwa na askari polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa shtaka la mauaji ya muongozaji wa filamu, Athuman Nyanza. Picha na Hadija Jumanne.
Akimsomea shtaka hilo, Wencelaus alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, kinyume na kifungu kifungu196 na kifungu 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Alidai, Rehema anadaiwa Februari 10, 2026 eneo la Mwapemba lililopo Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam, alimuua Athuman Nyanza.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wa kesi hii umekamilika” alidai wakili Wencelaus
Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 13, 2026 kwa kutajwa na mshtakiwa amepelekwa rumande.