
Washauri wa Rais Donald Trump wa Marekani wanazidi kuwa na wasiwasi kwamba kupanda kwa bei ya mafuta ya ndege kunakosababishwa na vita vya nchi hiyo na Israel dhidi ya Iran kutawadhuru Warepublican katika uchaguzi wa katikati ya muhula.
Gavana wa zamani wa New Hampshire, Chris Sununu, ambaye sasa anaongoza kundi la sekta ya ndege la Airlines for America, hivi majuzi alimuonya Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent kwamba bei za tiketi, ambazo tayari ziko juu, zitapanda zaidi ikiwa vita dhidi ya Iran vitaendelea.
Sununu amekuwa akiwaonya maafisa wa utawala wa Trump kuhusu mdororo wa kiuchumi unaosababishwa na mzozo huo, akisema kwamba vita lazima vikomeshwe haraka, la sivyo hali itazidi kuwa mbaya.
Wakati huo huo, jarida la Wall Street limeripoti kuwa, washauri wa Trump wanaogopa kwamba Warepublican watalipa gharama ya kisiasa kutokana na kupanda gharama za mafuta, na wengi wana hamu ya kukomeshwa vita kwa matumaini kwamba bei zitaanza kushuka kabla ya uchaguzi wa katikati wa muhula, Novemba mwaka huu.
Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyoanza mwishoni mwa Februari, vimevuruga pakubwa usafirishaji wa baharini kupitia Lango-Bahari la Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa meli kwa ajili ya usambazaji wa nishati duniani. Kufungwa lango hilo kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na mafuta ya ndege, na kuwaacha watumiaji wa vyombo hivyo huko Marekani wakikabiliana na gharama kubwa, wakati msimu wa usafiri wa kiangazi unapokaribia.
Bei ya mafuta ya ndege iliongezeka maradufu katika wiki chache zilizofuata kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, na imeendelea kuwa juu. Mashirika ya ndege yamesema gharama za ziada zitaongeza mabilioni ya gharama zao mwaka huu.