
Uchunguzi mpya wa maoni unaonyesha kuwa Wamarekani wengi wamepinga vikali picha iliyotengenezwa na Donald Trump kwa kutumia akili mnemba (AI) ikimdhihirisha kiongozi huyo kama Yesu Kristo, na vilevile matamshi yake yanayomshambulia Papa Leo XIV, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na Washington Post, ABC News na Ipsos unaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wamarekani hawakubaliani na maoni ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump kuhusu Papa Leo XIV, huku upinzani ukizidi kuwa mkubwa dhidi ya picha iliyotengenezwa kwa akili mnemba inayomonyesha Trump kama Yesu Kristo.
Uchunguzi huo wa maoni umebaini kuwa karibu Wamarekani 9 kati ya 10, au 87%, wana maoni hasi kuhusu picha ambayo Trump alichapisha kwenye Truth Social mnamo Aprili 12. Utafiti huo, uliofanywa kati ya Aprili 24 na 28, pia ulichunguza maoni ya umma kuhusu jinsi Trump anavyoshughulikia vita vya Iran, uchumi na gharama ya maisha.
Picha hiyo iliyotengenezwa kwa akili mnemba (AI) ilimdhihirisha Donald Trump akiwa amevaa majoho ya rangi nyeupe na nyekundu, akiweka mkono kwenye paji la uso la mgonjwa huku mwanga ukitoka kwenye mkono wake mwingine.
Wakosoaji wameitaja picha hiyo inayomuonyesha Trump kama Yesu Kristo kuwa inamvunjia heshima Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu na kudhihaki mafundisho ya dini. Kitendo hicho kimeibua upinzani kwenye duru za kidini na kisiasa Marekani na kwengineko duniani, na hata kutajwa kuwa ni ukafiri.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanaonyesha kuwa, 80% ya wapiga kura wa Trump na 79% ya chama cha Republican pia wamepinga picha hiyo. Muda mfupi kabla ya kuichapisha, Trump alikuwa amechapisha ujumbe mrefu akimshambulia Papa Leo, ambaye alikuwa amekosoa vita dhidi ya Iran. Trump alisema kwamba hana haja ya Papa ambaye anapinga sera zake.