Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mashambulizi yanayoongezeka ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, ikiyataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji vita na sheria za kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hamas imesema: Kuongezeka mashambulizi ya jeshi linalotenda jinai la Israel dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza na kulipuliwa kwa mabomu vitongoji vya Al-Darj na Al-Zaytoun katika Jiji la Gaza na eneo la Al-Mawasi magharibi mwa Khan Yunis, ambako kumepelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa, kunaonyesha azma ya adui ya kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa Sharm El-Sheikh sambamba na mwendelezo wa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo inasema: Utawala ghasibu wa Israel unaendeleza uhalifu wake wa kikatili dhidi ya Wapalestina chini ya kifuniko cha makubaliano ya kusitisha mapigano, bila ya kukabiliwa na jibu lolote la kuzuia ukiukaji huu mkubwa wa makubaliano na sheria za kimataifa.

Hamas imeongeza kuwa: Serikali ya Marekani na washirika wake wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuudhibiti utawala huo vamizi na kuulazimisha kusimamisha uchokozi dhidi ya raia wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.

Mwishoni mwa taarifa hiyo, harakati ya Hamas imesema: Tunatoa wito kwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake, zikiongozwa na Baraza la Usalama, kuchukua misimamo inayohakikisha ulinzi wa watu wa Palestina na kuzuia mashine ya mauaji ya Wazayuni dhidi ya raia wa Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *