Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana nchini kuhakikisha matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana hayajirudii tena, akisema yamelitia doa Taifa na kuharibu taswira ya nchi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 8, 2026 jirani na Uwanja wa Ndege wa Dodoma msafara wake uliposimamishwa na vijana waliobeba mabango yenye jumbe za “Never Again” (Yasijirudie tena).
“Niwaombe sana vijana, katika miji yenu, katika kazi zenu, katika shughuli zenu zote, ambizaneni yaliyotokea yasijirudie tena, kwani yamelitia doa Taifa letu,” amesema.
Amesema matukio hayo si sehemu ya hulka ya Watanzania na kusisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha amani inaendelea kutawala nchini kwa kulindana, kuelimishana na kuzuia vitendo vya fujo katika maeneo yao.
Katika mkutano huo, wananchi walitumia nafasi hiyo kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo mikopo, usafiri na mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo.
Akizungumzia suala la mikopo kwa vijana na wajasiriamali, Rais Samia amesema Serikali imeanza hatua za kusimamia utoaji wa mikopo kupitia taasisi nyingi zaidi za kifedha tofauti na ilivyokuwa awali, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa vijana na makundi mbalimbali ya wananchi.
Amesema mahitaji ya mikopo kwa vijana ni makubwa na kwamba Serikali itaendelea kuongeza rasilimali kadri uchumi utakavyoruhusu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali itatathmini uwezekano wa kuanzisha soko jingine la wafanyabiashara wadogo pembezoni mwa Soko la Machinga Complex jijini Dodoma ili kuongeza fursa za biashara, kupunguza msongamano na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.
Awali, wawakilishi wa wafanyabiashara wadogo walimweleza Rais Samia kuwa Soko la Machinga Complex limekuwa mfano mzuri wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kupanga biashara ndogondogo katika maeneo rasmi na salama.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mjumbe wa Shina namba 1 CCM Chamwino akishiriki kikao cha kawaida kilichoitishwa na Balozi wa Shina hilo, Paulina Mkasanga, leo Ijumaa Mei 8, 2026 Chamwino mkoani Dodoma.
Hata hivyo, waliomba kuboreshwa kwa huduma za usafiri wa daladala kuelekea sokoni hapo na kuimarishwa kwa uratibu wa biashara na huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo.
Kwa upande wao, mamalishe na babalishe waliomba masharti ya mikopo kwa makundi maalumu yaendelee kuboreshwa ili wananchi wengi zaidi wa kipato cha chini wanufaike.
Nao maofisa usafirishaji, wameihakikishia Serikali kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali katika kulinda amani na kuzuia matumizi mabaya ya vyombo vya usafiri kwa vitendo vya fujo.
Rais Samia amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Dodoma kufanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa na wananchi na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji atakaporejea mkoani humo.