Dar es Salaam. Kuzinduliwa kwa toleo la kwanza la mpango wa hatifungani ya Nyumba ya Kampuni ya Mikopo ya Nyumba ya Tanzania (TMRC), kumetajwa kutarahisisha upatikanaji wa nyumba kwa Watanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya TMRC, Elibariki Ndossi amesema kuzinduliwa kwa hatifungani hiyo kunasogeza mnyororo mzima wa kujenga, kununua au kumalizia nyumba kupitia taasisi za fedha na benki zinazotoa mikopo ya aina hiyo ambazo TMRC inashirikiana nazo.

Ameyasema hayo leo Mei 6, 2026 kwenye uzinduzi wa mpango wa pili wa hati fungani ya muda na kati pamoja na uzinduzi wa toleo la kwanza la mpango wa TMRC Nyumba Bond hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Amesema kazi kubwa ya TMRC ni kutafuta vyanzo vizuri vya fedha za muda mrefu na bei nafuu, kukopesha benki na taasisi za kifedha ambazo zinakwenda kukopesha mikopo rejareja kwaajili ya wananchi kujenga, kununua au kumalizia nyumba.

“Toleo hili la kwanza tunatatajia kukusanya takrbani Sh20 bilioni na tinawahamasisha wananchi wajaribu kutumia fursa hii kwaajili ya kujipatia kipato, riba ni asilimia 11 kwa mwaka na marejesho italipwa mara mbili kwa mwaka,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Yamungu Kayandabila, amesema kwa maendeleo ya sekta ya makazi nchini hatua hiyo ya uzinduzi ni muhimu.

“Uhitaji wa nyumba ni mkubwa TMRC inataka kututoa huko kama Shirika la Nyumba la NHC linavyosema maisha ni nyumba,” amesema Kayandabila ambaye amemuwakilisha Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba. 

Akimuwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama, Mkurugenzi wa usimamizi na uchunguzi wa Mamlaka hiyo, Exaud Julius amesema idhini imetolewa baada ya TMRC kukidhi vigezo.

“Dira ya taifa ya maendeleo inaelekeza kuwa na uchumi shindani, himilivu na shrikishi kwa Watanzania wote. Tunaamini fedha zitakazopatikana zitakwenda kuchochea miradi itakayowezesha kujenga nyumba na kuwa na makazi bora mwa Watanzania,” amebainisha.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya TMRC, Theobald Sabi amesema wanaihakikishia Serikali na wadau wote kuwa taasisi hiyo itazingatia usimamizi madhubuti ya rasilimali ili kulinga masilahi ya wawekezaji na Watanzania kwa ujumla.

Amesema Nyumba Bond inakwenda kuongeza uwezo wa kampuni katika kutoa mikopo kwa benki kwenye sekta ya nyumba huku akiwakaribisha wananchi, kampuni, wawekezaji na taasisi nchini.

“Lengo ni kuona wananchi wanakuwa na uwezo wa kupata makazi bora kupitia mikopo iliyo nafuu na ya muda mrefu,” amessma Sabi.

Akitoa hofu kwa wawekezaji amesema kampuni hiyo inasimamiwa na kumilikiwa na wadau wakubwa hivyo TMRC lazima itarudisha kwao.

Akieleza zaidi Sabi amefichua kuwa Serikali ya Tanzania imechykua hatua ya kuwekeza TMRC na sasa inamiliki asilimia 27.7.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *