
Musoma. Mkoa wa Mara umeunda bodi ya wadhamini kwa ajili ya kufufua timu ya Soka ya Biashara United ambayo awali iliweza kupanda hadi kushiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kwa misimu mitatu kabla ya kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo hali ngumu ya kiuchumi.
Bodi hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho imeundwa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya mkoa kuinua na kuibua vipaji katika sanaa na michezo ili kuleta burudani sambamba na kuboresha uchumi wa mkoa na watu wake.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumamosi, Mei 9,2026 wakati wa kupokea tuzo ya mbunifu wa mavazi ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Mara, Rosemary Range, Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi amesema pia mikakati hiyo ya mkoa inalenga kutoa fursa za ajira hususani kwa vijana kupitia sanaa na michezo.
“Mkoa wa Mara una vipaji vingi,ndio maana tumeona tuanze na soka kwani kupitia soka vijana wetu watapata ajira,watu wetu watapata burudani wakati huo huo pia uchumi wa mkoa na watu wake utapanda hasa pale timu kubwa kubwa zitakapokuwa zinakuja kucheza huku kwetu,” amesema Kanali Mtambi.
Hata hivyo Kanali Mtambi hakuwa tayari kueleza mikakati iliyopo kwa ajili ya kufufua timu hiyo huku akisema lengo kuu la bodi hiyo ni kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu na kumaliza ligi ikiwa katika nafasi za juu na si vinginevyo.
“Mikakati ipo mingi lakini kwa sasa naomba nisiizungumzie kikubwa ni kwamba tunataka kuwa na timu yetu ya mkoa itakayoshiriki ligi kuu na mashindano mengine. Mipango iko vizuri ikishakuwa tayari tutawaleza,” amesema
Akizungumza kuhusu mbunifu huyo wa mitindo, Kanali Mtambi amempongeza kwa ushindi huo alioupata kwa maelezo kuwa ushindi huo ni wa mkoa mzima.
Amewataka wasanii, na watu wengine kujitokeza kutumia talanta zao kwa ajili ya kuutangaza mkoa na kwamba Serikali ya mkoa iko tayari kuwaunga mkono.
“Haya ndiyo mambo tunayoyataka. Zamani Mara ilikuwa ikijulikana kwa mambo mabaya lakini leo mwanamitindo wetu ametutangaza kimataifa. Nitoe wito kwa wengine wengi kujitokeza na kuwa mabalozi wema wa mkoa wetu kwani uwezo wa kufanya hivyo upo kinachotakiwa ni nia na uthubutu,” amesema
Akizungumza kuhusu tuzo hiyo,mwanamitindo huyo amesema mashindano hayo ya ubunifu wa mavazi yalifanyika nchini Kenya na kushirikisha washiriki kutoka nchi 15 za Afrika na yeye kuibuka mshindi.
Range amesema watanzania wanapaswa kutoa ushirikiano kwa mabinti wenye nia ya kuwekeza kupitia tasnia uanamitindo na urembo kwa maelezo kuwa tasnia hizo zina mchango mkubwa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
“Kuna watu bado wanafikiri kuwa urembo na uanamitindo ni uhuni, hii dhana haina ukweli hii ni ajira kama zilivyo ajira zingine,wazazi, walezi na jamii tunapaswa kuwaunga mkono watoto wetu wanaotamani kuwa wanamitindo tusiwakatishe tamaa,” amesema
Amesema tuzo hiyo imemuongezea hamasa ya kufanya vizuri katika shughuli zake huku lengo lake likiwa ni kuitangaza nchi ya Tanzania kimataifa zaidi.