Morogoro. Wakuu wa Taasisi za mafunzo na utafiti kwenye sekta ya kilimo na mifugo wametakiwa kujitambua kwamba wao ni viongozi na wanapaswa kujua namna sahihi ya kutatua migogoro inayoweza kutokea kwenye taasisi zao na kuleta usawa baina yao na watumishi wanaowaongoza.

Hayo yamesemwa leo Mei 9, 2026 mkoani Morogoro na mkufunzi kutoka Eminent Corporate Academy, Dk Kelvin Mwita ambaye ni mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo ya uongozi na usimamizi wa taasisi yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la kilimo endelevu (SAT) na kuwahusisha wakuu wa Taasisi za mafunzo na utafiti kwenye sekta ya kilimo na mifugo.

Dk Mwita amesema taasisi inapoingia kwenye mgogoro na jamii, watendaji wa taasisi ama wateja wakuu wa Taasisi hizo wasiangalie kwenye kushinda migogoro hiyo bali waangalie kwenye kuzifanya taasisi ziwe na amani, utulivu na uendelevu.

“Kabla ya kutoa mafunzo haya tumeangalia mahitaji yaliyopo kwenye taasisi hizi hasa katika masuala ya uongozi, usimamizi wa taasisi na utawala bora, hivyo mada zetu zimelenga mahitaji ya taasisi hizi,” amesema Dk Mwita.

Ametaja baadhi ya mada hizo kuwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro ndani ya taasisi, ushirikiahwaji, maandalizi ya maisha baada ya kustaafu na usimamizi wa rasilimali za taasisi.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo meneja miradi kutoka SAT, Kashindye Salumu amesema mafunzo hayo ya wiki moja yamehususha wakuu wa Taasisi za mafunzo na utafiti hapa nchini wapatao 48 pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Kilimo na Mifugo.

Amesema mafunzo hayo yamelenga kuimarisha masuala ya uongozi kwenye taasisi ili wakuu hao wasimamie vema rasilimali watu kwenye taasisi zao lakini pia kuweza kusaidia utatuzi wa migogoro inayoweza kujitokeza kwenye taasisi zao.

“Mafunzo haya yametolewa kupitia mradi wa ‘kuwezesha utekelezaji wa mafunzo’ ulioanza 2019 ambapo umejikita kwenye sekta ya kilimo na mifugo kupitia wizara husika,” amesema Salum.

Wakuu wa taasisi wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani yameweza kuwaimarisha na kuwaongezea ujuzi wa kusimamia taasisi na kushughulikia migogoro inayoweza kujitokeza kwenye taasisi zao.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro, Witness Bashaka amesema pamoja na SAT kuwapa mafunzo ya mara Kwa mara lakini mafunzo ya sasa yamekuwa na utofauti Kwa sababu yanwwafanya waweze kujitambuka kuwa wao ni viongozi na wajibu wao.

Naye, kaimu mkuu wa idara ya taaluma saidizi kutoka wakala wa mafunzo ya mifugo (Lita), Dk Bakari Ngecha amesema mbali ya kupewa mafunzo hayo, SAT wamesaidia katika kuandaa mitaala mipya mitatu ya kufundishia baada ya ile iliyokuwepo awali kuonekana imepitwa na wakati.

Amesema mafunzo hayo ya uongozi na usimamizi yataleta tija kubwa kwenye taasisi yake kwa kuwa yataimarisha dhana ya utawala bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *