
Mwakilishi wa Bunge la Ulaya ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mauaji yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya wasichana wa Shule ya Msingi ya Minab kusini mwa Iran, akisema huenda yalikuwa shambulio la kupangwa.
Akizungumza katika mkutano wa mazishi uliopewa jina la Malaika wa Minab, uliofanyika nje ya ubalozi wa Iran huko Brussels, Milan Uhrik amesema anashuku kwamba shambulio hilo lilifanywa kwa makusudi.
“Shambulio dhidi ya shule ya msingi huko Minab lazima lichunguzwe,” amesema mbunge huyo wa Bunge la Ulaya.
Ametaja mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kama mfano wa kile ambacho wanajeshi wa utawala wa Israel wanawafanyia raia wa kawaida. Uhrik amesema mashambulizi yanayowalenga watoto, wanawake na wazee wa Lebanon ni mifano mingine ya ukatili wa askari wa Israel.
Mwakilishi huyo wa Bunge la Ulaya amesema, mashambulizi ya anga dhidi ya Shule ya Msingi ya Minab ni uhalifu wa kivita, na Umoja wa Ulaya haunapaswi kuwa mshirika katika vitendo hivyo vya uhalifu.
Mwanasiasa huyo wa Kislovakia ameikosoa Tume ya Ulaya na viongozi wa nchi za bara hilo kuwa wanatumia sera za kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na uhalifu kama huo.
Amesema Wazungu wanajaribu kuepuka uchunguzi kuhusu uhalifu huu kwa sababu ni dhaifu, akiongeza kuwa viongozi wa Ulaya hawawezi kuonyesha upinzani dhidi ya sera za ukatili zinazoongozwa na Washington na Tel Aviv.
Marekani na Israel zilianzisha vita visivyo na uchochezi dhidi ya Iran mnamo Februari 28, na kuwaua watoto na zaidi ya walimu 168 katika mashambulizi ya anga kwenye Shule ya Minab kusini mwa Iran katika siku ya kwanza ya vita hivyo.