
Afisa mwandamizi wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen ameonya kuwa Marekani italazimika kubeba dhima ya madhara ya kukataa mapendekezo mapya ya Iran ya kumaliza vita, kufuatia matamshi ya kupinga yaliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Nasruddin Amer, naibu mkuu wa ofisi ya habari ya Ansarullah, aliandika katika ukurasa wake wa X kuwa:
“Tangu mwanzo, ilionekana wazi kutokana na maandalizi ya kijeshi ya Marekani na msimamo wake mgumu kwamba hawatakubali majibu ya Iran. Kwa hiyo, wanabeba wao wenyewe wanabebe dhima ya madhara yawe makubwa au madogo.”
Amer alibainisha kuwa kukataliwa kwa majibu ya Iran kulitokea muda mfupi baada ya mawasiliano ya Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye alimemtaja kama “mhalifu”.
Mapendekezo ya Iran, yaliyowasilishwa kupitia wasuluhishi wa Pakistan, yalifikishwa Washington siku ya Jumapili.
Kwa mujibu wa ripoti ya IRIB, pendekezo hilo lilisisitiza ulipaji wa fidia kamili ya uharibifu wa vita na kuondolewa kwa vikwazo vyote. Pia lilitaka kuachiliwa kwa mali za Iran zinazoshikiliwa kwa amri ya Marekani na kutambuliwa kwa mamlaka ya Iran juu ya Mlango wa Hormuz.
Wakati huo huo, Trump alijibu vikali baada ya kupokea majibu ya Tehran akiyaita kuwa “hayakubaliki kabisa.”
Katika mahojiano na Axios, Trump alisema pia kuwa amejadiliana kuhusu majibu ya Iran na Netanyahu.
Wachambuzi wa masuala ya nishati na usalama wa bahari wanasema kuwa ikiwa Mlango wa Bab el‑Mandeb, unaodhibitiwa na Yemen, ambao umekuwa njia mbadala tangu Iran ilipoimarisha udhibiti wake katika Hormuz, utafungwa pia, basi usafirishaji wa mafuta ya Saudi Arabia kupitia bandari zake za magharibi unaweza kusimama.
Hatua kama hiyo ya Yemen inaweza kusababisha kupanda zaidi kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa, ambayo tayari imeongezeka maradufu ikilinganishwa na kipindi kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.