Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Paris haijawahi kufikiria kupeleka vikosi vya kijeshi vya Ufaransa katika Mlango-Bahari wa Hormuz bila uratibu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wakati mvutano unaochochewa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran ukiendelea.

Akizungumza Jumatatu katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari jijini Nairobi pamoja na Rais wa Kenya William Ruto, Macron amesisitiza kuwa Ufaransa haikuwahi kupanga hatua ya kijeshi ya upande mmoja katika njia hiyo muhimu ya bahari.

Macron aliwaambia waandishi wa habari ppelekaji wa jeshi la Ufaransa kukabiliana na Iran haujawahi kufikiriwa.

Hata hivyo, alieleza kuwa Paris iko tayari kutoa msaada “kwa uratibu na Iran” ili kusaidia kurejesha usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz, ambao ni njia nyeti kwa usafirishaji wa nishati duniani.

Kuhusu kupelekwa kwa meli kubwa ya kivita ya kubeba ndege ya Ufaransa, Charles de Gaulle, katika Bahari Nyekundu, Macron alisema hatua hiyo inahusiana na kuongezeka kwa mvutano wa kiusalama katika eneo hilo.

Kauli za Macron zimekuja wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa onyo kali dhidi ya uwepo wa meli za kivita za Ufaransa, Uingereza, au nchi nyingine yoyote karibu na Mlango wa Hormuz. Tehran imesisitiza kuwa harakati zozote za kijeshi katika eneo hilo lazima zifanyike kwa uratibu na Iran.

Hadi sasa, juhudi za kidiplomasia za kurejesha utulivu katika njia hiyo muhimu ya bahari ambayo hupitisha kiwango kikubwa cha mafuta na gesi ya dunia, zimeripotiwa kukwama kutokana na ukaidi wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *