
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amejadiliana na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Misri kuhusu maendeleo muhimu katika mchakato wa kidiplomasia kati ya Iran na Marekani unaopatanishwa na Pakistan.
Araghchi alifanya mazungumzo ya simu tofauti Jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, na mwenzake wa Misri, Badr Ahmed Mohamed Abdelatty.
Mazungumzo kati ya mwanadiplomasia mkuu wa Iran na mwenzake wa Saudi yalikuwa mawasiliano yao ya pili ndani ya kipindi cha saa 24, ishara ya kuongezeka kwa mashauriano ya kikanda katika wakati huu wa mvutano wa kisiasa na kijeshi.
Katika mazungumzo yake na Abdelatty, Araghchi pia aligusia matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi na athari zake kwa usalama wa kikanda.
Siku ya Jumapili, waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran pia alibadilishana mawazo na mawaziri wa mambo ya nje wa Qatar na Uholanzi kuhusu masuala muhimu yanayoendelea katika eneo.
Mazungumzo hayo ya simu yalifanyika siku moja baada ya Iran kuwasilisha kwa Pakistan majibu yake kuhusu pendekezo la Marekani la kumaliza vita vinavyoendelea. Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump alikataa majibu hayo, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa.”
Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema pendekezo la Iran la kumaliza vita vya hivi karibuni lilikuwa la busara, huku Marekani ikiendelea kusisitiza “matakwa yasiyo na msingi” yaliyoundwa na utawala haramu wa Israel.
Akizungumza katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari Jumatatu, Baghaei alijibu maswali kuhusu jinsi serikali ya Marekani ilivyopokea pendekezo la Iran. Amesema: “Hatukudai chochote cha ziada. Kitu pekee ambacho tumedai ni haki halali za Iran.”
Baghaei amesema kilo ambacho Iran inataka ni kukomeshwa kwa vita katika eneo, kusitishwa kwa uharamia wa baharini dhidi ya meli za Iran, na kuachiliwa kwa mali za wananchi wa Iran ambazo zimezuiliwa isivyo haki kwa miaka mingi.