Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, ameitaka Wizara ya Afya kuanzisha kitengo maalumu cha kutoa elimu ya afya mitandaoni ili kudhibiti taarifa potofu zinazotolewa na baadhi ya watu wasiokuwa wataalamu.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni Dodoma leo Jumanne, Mei 12, 2026 Baba Levo amesema kumekuwa na ongezeko la watu wanaotoa ushauri wa afya kupitia mitandao ya kijamii hali inayowachanganya wananchi.

Amesema baadhi ya ushauri unaotolewa hauzingatii hali halisi ya maisha ya Watanzania wengi hasa wa vijijini ambao chakula kikuu ni ugali.

Mbunge huyo amesema wakati mwingine wananchi hupokea taarifa zinazokinzana kuhusu vyakula, ambapo mtu mmoja anashauri kula matunda huku mwingine akivikataza kwa madai vina sukari nyingi.

Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua watu wanaotoa elimu ya afya bila utaalamu na kuanzisha mfumo rasmi wa utoaji wa taarifa sahihi mtandaoni.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Micheweni, Hamis Vuai amesema China tayari imeweka utaratibu unaoruhusu ushauri wa afya kutolewa na watu wenye sifa na waliothibitishwa na mamlaka husika pekee.

Endelea kufuatilia Mwananchi…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *