
Unguja. Mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said (CCM) amesema wakuu wa mikoa na wilaya wanatumia sheria vibaya kuwaweka watu kizuizini bila sababu za msingi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Mikoa ya 1962 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kifungu cha 7 (1) kinampa mamlaka mkuu wa wilaya au mkoa kumuweka mtu mahabusu bila kwenda mahakamani kwa saa 48.
Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, leo Jumanne, Mei 12, 2026 Simai amesema watendaji hao wanatakiwa kutambua wajibu wao na wasitumie.
“Hii sheria imewapa mamlaka lakini wakuu wa mikoa na wilaya wanaitumia vibaya na kuwanyanyasa wananchi kuwaweka vizuizini bila sababu maalumu,” amesema.
Simai amesema sheria hiyo iwape nguvu kubwa na kutaka kumwadhibu mtu bila sababu za msingi na kutumia mabavu kuwanyanyasa wananchi.
Kuhusu usafi wa mji, mwakilishi huyo amesema bado ni mchafu jambo ambalo linaondoa haiba ya Zanzibar ikizingatiwa ni jiji la kitalii.
Mwakilishi Moza Mohamed Khamis nafasi za wanawake, amesema kuna changamoto kubwa kwa wananchi kupata vitambulisho vya Mzanzibari na wakati mwingine imekuwa kama haramu.
“Hivi vitambulisho ni halali kwa kila Mzanzibari, lakini kumekuwapo na ukiritimba kupata vitambulisho hivi watu wanazungushwa bila sababu za msingi, tunapaswa kutambua kwamba nchi hii ni yetu sote na watu wote wana haki sawa hakuna mwenye haki kuliko mwingine,” amesema Moza.
Mwakilishi wa Wete, Shafi Mohamed Shafi (ACT) amesema vikosi vya SMZ vimeamua kufanya kazi ya polisi na kuwanyanyasa wananchi bila kuzingatia misingi ya utendaji kazi.
Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih (ACT- Wazalendo), amesema wizara kwa sasa badala ya kuwa faraja zimekuwa kero na kuwanyanyasa wananchi.
Akijibu hoja za wawakilishi hao wakati akihitimisha hoja, waziri mwenye dhamana, Idrissa Kitwana Mustafa amesema atakwenda kukaa pamoja na wakuu wa wilaya na mikoa ili kuangalia namna nzuri wanapofanya shughuli zao.
Kuhusu vitambulisho, amesema wapo baadhi ya wananchi ambao hawataki kufuata utaratibu na wakati mwingine wananchi hukosea majina yao, hivyo wanapotaka kubadilishwa wanatakiwa kulipia.
Kuhusu uchafu amesema katika bajeti hii wanatarajia kujenga vizimba 111 vya Unguja na Pemba na kutakuwepo na kampuni na magari ya kisasa kwa ajili ya kuimarisha usafi.
Baraza limepitisha makadirio ya mapato na matumzi ya Sh697.7 bilioni.