Madrid, Hispania. Kocha mwenye mafanikio makubwa barani Ulaya, José Mourinho, yupo mbioni kurejea tena kuinoa Real Madrid, huku akiweka masharti kabla ya kurudi kwa mara nyingine tena ndani ya viunga vya Bernabeu.
Sharti la kwanza, Mourinho anataka apewe mamlaka ya mwisho kuhusu hatma ya viungo Aurélien Tchouaméni na Federico Valverde baada ya wawili hao kuripotiwa kugombana mazoezini.
Pili, Mourinho anataka usajili mpya wa kuimarisha kikosi katika maeneo kadhaa akiamini timu ya sasa haina uwiano mzuri kikosini.
Viungo wa Real Madrid, Aurélien Tchouaméni (kulia) na Federico Valverde (kushoto) ambao waliripotiwa kugombana mazoezini wiki iliyopita. Picha na Mtandao
Taarifa kutoka Hispania zinaeleza kuwa rais wa Madrid, Florentino Pérez, tayari ameanza mazungumzo binafsi na Mourinho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Álvaro Arbeloa mwishoni mwa msimu huu.
Inaelezwa kuwa Madrid inaweza kumpata Mourinho kwa ada ya paundi 2.6 milioni (Sh9 bilioni) pekee endapo itakamilisha dili hilo ndani ya siku 10 baada ya mchezo wa mwisho wa Benfica msimu huu dhidi ya Estoril utakaochezwa Mei 16.
Katika kipindi chake cha kwanza Santiago Bernabéu, Mourinho aliipa Madrid ubingwa wa La Liga, Copa del Rey na Spanish Super Cup, huku akionyesha ushindani mkubwa dhidi ya Barcelona iliyokuwa chini ya Pep Guardiola.
Meneja wa Benfica, Jose Mourinho (kulia), akiwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo (kushoto) wakati wawili hao walipokuwa wakihudumu Santiago Bernabeu. Picha na Mtandao
Ripoti hizo zinaeleza kwamba Mourinho anaamini bado ana kazi ambayo hajamaliza Madrid, hasa baada ya kushindwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo alipokuwa kocha wa timu hiyo.
Pia imeelezwa kuwa kocha huyo mwenye miaka 63 yupo tayari kukataa ofa kutoka Chelsea kwa ajili ya kurejea Hispania.
Mourinho kwa sasa anaelekea kumaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote akiwa Benfica, jambo lililomfanya kuwa chaguo namba moja kwa mabosi wa Madrid licha ya kuwa aliwahi kuinoa klabu hiyo mwaka 2010 hadi 2013.
Madrid inatajwa kutaka kumtambulisha Mourinho rasmi kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia huku mazungumzo yakitarajiwa kushika kasi mara baada ya msimu wa ligi kumalizika.