Kibaha. Miti 3,000 imepandwa katika shule 10 za msingi na sekondari Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, katika kampeni maalumu ya kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi inayoendeshwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Katika Shule ya Msingi Amani, jumla ya miche 90 ya miti ya kivuli ilipandwa leo Mei 12, 2026 na NEMC Kanda ya Mashariki na Kaskazini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa shughuli ya upandaji miti hiyo leo , Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki na Kaskazini, Glory Kombe amesema hatua hiyo inalenga kurejesha mazingira yaliyoharibika na kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

“Tunashuhudia uoto wa asili ukipungua kwa kasi kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo tumeona ni muhimu kuhamasisha upandaji wa miti mashuleni ili kizazi cha sasa na kijacho kiwe sehemu ya suluhisho,” amesema Kombe.

Amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha miti hiyo inatunzwa vizuri ili iweze kukua na kuleta manufaa kwa jamii na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake, mwalimu wa idara ya mazingira katika Shule ya Msingi Amani, Kikwesha Aron amesema shule hiyo imeweka mikakati maalumu ya kuhakikisha miti yote iliyopandwa inastawi.

“Tumewagawa wanafunzi wawili kwa kila mti ili wawe na jukumu la kuuhudumia, kuumwagilia na kuhakikisha unakua vizuri. Tunaamini mpango huu utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa wanafunzi katika utunzaji wa mazingira,” amesema Aron.

Ametoa shukrani kwa NEMC kwa kuichagua shule hiyo kuwa sehemu ya kampeni hiyo ya mazingira akieleza kuwa miti hiyo itasaidia kuongeza kivuli na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Naye mwanafunzi wa shule hiyo, Abdul Nasri amesema ujio wa miti hiyo ni hatua muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa sababu miti ina mchango mkubwa katika maisha ya binadamu.

“Miti hutusaidia kupata hewa safi, kivuli na kulinda mazingira yetu. Tunashukuru kwa kuletwa miti hii na sisi tutajitahidi kuitunza ili ikue,” amesema Abdul.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *