Chanzo cha picha, @modgovksa/X
Baada ya kuripotiwa jana kuwa UAE ilifanya mashambulizi ya siri ya anga dhidi ya Iran, shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba Saudi Arabia pia ilitekeleza mashambulizi kadhaa ambayo hayakutangazwa rasmi dhidi ya Iran, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake wakati wa vita vya Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Magharibi wenye ufahamu wa suala hilo pamoja na maafisa wawili wa Iran, mashambulizi hayo ndiyo mara ya kwanza kwa Saudi Arabia kujulikana kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kijeshi ndani ya ardhi ya Iran, hali inayotafsiriwa kuwa ishara ya Riyadh kuonyesha uthubutu zaidi katika kujilinda dhidi ya mpinzani wake mkuu wa kikanda.
Reuters imesema katika ripoti yake maalumu kuwa mashambulizi hayo, ambayo hayajawahi kuripotiwa hapo awali, yalifanywa na jeshi la anga la Saudi Arabia na huenda yalitekelezwa mwishoni mwa mwezi Machi.
“Hayakuwa mashambulizi ya kawaida, bali yalikuwa ya kulipiza kisasi baada ya Saudi Arabia kushambuliwa,” mmoja wa maafisa hao wa Magharibi aliliambia Reuters.
Hata hivyo, Reuters imesema haikuweza kuthibitisha maeneo mahsusi yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.
Afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia hakuzungumzia moja kwa moja madai hayo alipoulizwa na Reuters kutoa maoni, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran nayo ikikataa kujibu ombi la shirika hilo la habari.
Saudi Arabia, ambayo kwa muda mrefu imekuwa na ushirikiano wa karibu wa kijeshi na Marekani, imekuwa ikitegemea ulinzi wa Marekani dhidi ya vitisho vya kikanda. Hata hivyo, vita vya wiki 10 vilivyoikumba Mashariki ya Kati vimeonekana kuiacha nchi hiyo katika mazingira hatarishi baada ya baadhi ya mashambulizi kupenya mifumo ya ulinzi inayoungwa mkono na Marekani.
Jana, gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu ulifanya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Iran katika Ghuba ya Uajemi katika saa za mwanzo za tangazo la usitishaji mapigano kati ya Iran na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi hayo yalijumuisha angalau shambulizi moja dhidi ya vituo vya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran katika Kisiwa cha Lavan.
Soma zaidi: