
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amesema kuwa msimamo wa Marekani wa kutaka masharti ya kupita kiasi pamoja na mienendo yake mingine inayodhoofisha juhudi za diplomasia ndiyo vizuizi vikuu vya kumaliza mzozo uliozuka kufuatia vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mwanadiplomasia huyo mkuu alitoa kauli hiyo mjini Tehran Jumanne alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Andreas Motzfeldt Kravik, aliyefika katika mji mkuu wa Iran akiongoza ujumbe wa kidiplomasia kwa mashauriano na maafisa wa Iran.
Araghchi pia amesema kuwa matamshi ya vitisho na uchochezi kutoka Marekani, ukosefu wa nia njema pamoja na kutokuwa waaminifu ni miongoni mwa vikwazo vinavyozuia kupatikana kwa suluhu ya hali ya sasa na kufikiwa kwa makubaliano yanayowezekana.
Kwa ushirikiano na utawala wa Israel, Marekani ilianzisha duru yake ya hivi karibuni ya mashambulizi haramu dhidi ya Iran kuanzia Februari 28 hadi Aprili 7.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kusitishwa kwa mapigano tarehe hiyo ya mwisho kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran yaliyokuwa makali sana, lakini Aprili 13 akatangaza kuendelea kwa vizuizi dhidi ya meli na bandari za Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ilianza kuweka vizuizi katika Mlango wa Bahari wa Hormuz ,njia muhimu ya kimkakati kwa usafirishaji wa mafuta duniani , dhidi ya maadui wake na washirika wao mara baada ya kuanza kwa mashambulizi hayo. Tehran baadaye iliimarisha zaidi udhibiti huo kufuatia uamuzi wa Trump wa kuendeleza mzingiro huo wa kiuchumi na kijeshi.
Iran imeweka wazi kuwa haitarejea kwenye meza ya mazungumzo hadi Marekani itakapotekeleza masharti yake, yakiwemo kusitisha kile ilichokitaja kuwa uchokozi katika nyanja zote pamoja na kuondoa vizuizi hivyo.
Araghchi amesisitiza pia kuwa chanzo kikuu cha hali ya sasa katika Mlango wa Hormuz ni mashambulizi ya Marekani na Israel pamoja na ukiukwaji wa mara kwa mara wa usitishaji mapigano kupitia kuendelea kwa mzingiro huo.
Kwa upande wake, afisa huyo wa Norway amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa amani ya kudumu na utulivu katika eneo hilo pamoja na juhudi za kulinda sheria za kimataifa.
Pia alieleza utayari wa nchi yake kusaidia kuimarisha diplomasia pamoja na mashauriano kuhusu usalama wa baharini na ulinzi wa mazingira katika ukanda huo.