Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC imeanza ujenzi wa mradi mkubwa wa Kituo cha Tiba ya Moyo utakaosaidia kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Batilda Burian wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla ya chakula cha jioni itakayofanyika Jumamosi ya tarehe 30 mwezi huu kwa lengo la kuchangisha fedha za kusaidia ujenzi wa kituo hicho muhimu cha tiba ya moyo.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia wananchi wa mikoa ya kanda ya kaskazini kupata huduma za kibingwa kwa karibu zaidi, kupunguza gharama za matibabu pamoja na adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam kutafuta huduma hizo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahamasisha wananchi, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki harambee hiyo, akieleza kuwa mchango wa kila mmoja utakuwa sehemu ya kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo wanaohitaji huduma za haraka na za kitaalamu.
Kwa upande wake Afisa miradi na mipango WA KCMC Emmanuel Biachi meeleza kuwa kituo hicho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa vituo vya kisasa vitakavyotoa huduma za uchunguzi, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa wananchi wa ukanda wa kaskazini na maeneo jirani.
(Feed generated with FetchRSS)
