
Shinyanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, limekamata watuhumiwa 78 kwa makosa mbalimbali pamoja na silaha moja aina ya bastola ikiwa na risasi 11, iliyoripotiwa kuibiwa Mei 10, 2026 katika mtaa wa Nyakato wilayani Kahama.
Silaha hiyo ilikuwa mali halali ya Richard Mhabi, huku watu wawili wakishikiliwa kuhusiana na tukio hilo na tayari wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2026 wakati wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Jeshi la Polisi kwa Mei, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema wahamiaji haramu 11 pia wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa kuishi nchini bila vibali halali.
Amesema katika operesheni mbalimbali zilizofanyika mkoani humo, jeshi hilo pia limekamata vielelezo tofauti vikiwamo mafuta ya dizeli lita 480, mabati 558, kete 228 za bangi, lita 115 za pombe haramu ya moshi, kilogramu 89 za mirungi, pikipiki 11 na betri tatu za magari.
“Watuhumiwa 78 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali pamoja na silaha moja aina ya bastola TISAS yenye risasi 11 sambamba na vielelezo mbalimbali vilivyokamatwa katika operesheni hizo,” amesema.
Aidha, amesema jumla ya makosa 6,370 ya usalama barabarani yamebainika, huku madereva wanne wakifungiwa leseni kwa muda wa miezi mitatu kila mmoja kwa kosa la kuendesha kwa mwendo kasi wa kilomita 80 kwa saa.
Magomi, amesema Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwamo stendi, shule, maeneo ya ibada na makazi ya watu kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao wa kushiriki katika kulinda usalama wa jamii.
Kwa upande wake, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Paulo Mageni, amesema operesheni hizo zinaonyesha juhudi za Jeshi la Polisi katika kukabiliana na uhalifu na kurejesha hali ya usalama kwa wananchi.
“Tunapongeza kazi inayofanywa na polisi, hasa kukamata silaha ambazo ni chanzo cha matukio mengi ya uhalifu. Tunaamini hatua hizi zitasaidia wananchi kuendelea kuishi kwa amani,” amesema Mageni.
Rehema Nyalusi, amesema elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi kwa wananchi inapaswa kuendelea ili kusaidia jamii kushiriki katika ulinzi na kutoa taarifa za uhalifu mapema.
“Polisi wanapofika mashuleni, stendi na maeneo ya ibada kutoa elimu, wananchi wanapata uelewa wa namna ya kujilinda na kushirikiana na vyombo vya dola. Hii ni njia nzuri ya kupunguza matukio ya uhalifu,” amesema.
