Wawakilishi waikalia kooni Kampuni ya Rand Water tatizo la maji ZanzibarWawakilishi waikalia kooni Kampuni ya Rand Water tatizo la maji Zanzibar

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameikalia kooni kampuni ya Rand Water, wakidai imeshindwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji visiwani humo, huku wakisisitiza kuwa bila Serikali kuweka bajeti zinazotekelezeka, tatizo hilo litaendelea kuwaumiza wananchi.

Wawakilishi hao, wameeleza kuwa licha ya Serikali kuja na sera inayoruhusu ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika huduma za maji kupitia kampuni hiyo inayofanya kazi kwa ubia na Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), bado wananchi wengi wanaendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.

Hoja hizo zimetolewa leo Mei 29, 2026 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani, Unguja.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi wa Mtabile, Alley Masoud Alley (ACT-Wazalendo), amesema Serikali inapaswa kukubali kuwa Rand Water imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 “Maji ndio kila kitu na maisha yetu yanategemea maji. Rand Water ni tatizo, lazima tukubali,” amesema.

Naye, Mwakilishi wa Tumbe, Mmanga Mohamed Hamed, amesema changamoto ya maji inaenda sambamba na kukatika kwa umeme mara kwa mara jambo linaloendelea kuwaathiri wananchi.

“Hawa Rand Water wanatuchezea sana, hawatufai katika nchi, lazima Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru wananchi wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkwajuni, Sulubu Kidongo Amour (CCM), amesema malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa maji yamekuwa mengi lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa.

“Lazima tuseme ukweli, wananchi hawanufaiki na huduma ya maji. Kitu muhimu duniani ni maji lakini imekuwa tofauti kwetu, watu wanaangalia maslahi yao kwanza kuliko wananchi,” amesema.

Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT-Wazalendo), ametaka Serikali kueleza mchakato uliotumika kuipata kampuni hiyo pamoja na namna bili kubwa za maji zinavyotolewa kwa wananchi wasiopata huduma.

“Kuna mtu anapata bili ya maji mpaka Sh500,000 lakini hajawahi kupata huduma hiyo. Tunataka majibu ya Waziri kuhusu mambo haya,” amesema.

Naye Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Mkungu (CCM), amesema pamoja na kuwepo kwa maboresho ya huduma za maji ikilinganishwa na miaka ya nyuma, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Amesema utekelezaji wa mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Exim wenye thamani ya dola za Marekani milioni 92 unapaswa kuonekana kwa wananchi kupitia upatikanaji wa huduma bora.

“Kuna baadhi ya watendaji wana changamoto na wengine wanafanya hujuma, hivyo lazima wachunguzwe na kuchukuliwa hatua,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Pandani, Omar Fakih Hamad, amesema chanzo kikubwa cha changamoto hizo si Rand Water wala Zawa pekee, bali ni bajeti ndogo zinazotolewa kwa wizara hiyo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 wizara hiyo ilitengewa Sh220 bilioni lakini hadi sasa zimetolewa asilimia 39 pekee, hali inayofanya utekelezaji wa miradi ya maji na umeme kuwa mgumu.

“Huwezi kumaliza tatizo la maji au umeme kwa namna hii. Serikali lazima iweke bajeti zenye uhalisia na kutoa fedha kwa wakati,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *