Burna Boy anavyoiweka Afrika kwenye ramani ya muziki dunianiBurna Boy anavyoiweka Afrika kwenye ramani ya muziki duniani

Nigeria. Mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Burna Boy, 34, ameshirikiana na staa wa muziki wa Pop kutoka Colombia, Shakira, 49, katika wimbo mpya wa Kombe la Dunia 2026.

Burna Boy, mkali wa kibao cha On The Low (2018), hajaipata nafasi hiyo kwa bahati mbaya bali tayari alishakuwepo katika viwango vya kupata fursa kama hizo.

Shakira na Burna Boy wameshirikiana katika wimbo, Dai Dai (2026) ambao umechanganya mahadhi ya Afro-Latin na Afrobeats, huku ukihamasisha ustahimilivu na umoja. Huu ndio wimbo rasmi wa Kombe la Dunia la FIFA 2026, mashindano itakayoanza mnamo Juni katika nchi tatu za Amerika Kaskazini ambazo ni Marekani, Canada na Mexico.

BURN 01

Vilevile wimbo huu unaunga mkono FIFA Global Citizen Education Fund, mpango unaolenga kukusanya Dola100 milioni hadi kufikia mwishoni wa mashindano hayo ili kuwapatia watoto elimu na fursa za michezo.

Hii si mara ya kwanza kwa Burna Boy kuhusika katika matukio makubwa ya kimichezo, amefanya hivyo mara kadhaa ndani ya Afrika na hata nje ya bara hili.

Burna Boy alitumbuiza katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFACL) 2022/23, hatua iliyomfanya kuandika rekodi kama mwanamuziki wa kwanza kutoka Afrika kutoa burudani katika fainali hizo. Mbali na rekodi hiyo, pia iliripotiwa kuwa alipokea malipo ya Dola2 milioni, wastani wa Sh5 bilioni kwa sasa, kwa show hiyo aliyotumia takribani dakika 10 tu jukwaani.

BURN 02

Hatua hii ilimuongezea sifa kwani alitumbuiza mbele ya mashabiki 75,000 waliojitokeza katika uwanja wa Ataturk Olympic huko Instanbul, Uturuki kushuhudia fainali iliyowakutanisha Manchester City na Inter Milan.

Hata hiyo ya kutumbuiza fainali ya UEFA haikuwa bahati mbaya kwani Burna Boy ndiye msanii kutokea Afrika ambaye amekuwa akifanya show nyingi za kimataifa tena katika viwanja vikubwa na kujaza mashabiki wengi.

Juni 2023, Burna Boy aliandika historia kwa kuwa msanii wa kwanza kutokea Afrika kufanya tamasha kubwa katika uwanja wa London, Uingereza wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 80,000.

Mwaka mmoja baadaye akarejea tena katika uwanja huo na kufanya tamasha la pili lililovunja rekodi kwa kuuzwa tiketi zote.

Mbali na London Stadium, tayari Burna Boy amejaza viwanja, kumbi na arena kubwa kama State Farm Arena, Atlanta, Marekani (watu 21,000), Madison Square Garden, New York, Marekani (20,700), Accor Arena, Paris, Ufaransa (20,300), 02 Arena, London, Uingereza (20,000) n.k.

“Nimeuza tiketi zote 02 Arena pekee yangu, kwa bei niliyotaka, kwa njia niliyotaka. Kamwe usiongee sana, onyesha vitendo,” amesema Burna Boy mnamo 2021 baada ya show yake aliyofanya 02 Arena, London.

BURN 03

Kwa hiyo Burna Boy ni mwanamuziki mwenye ushawishi mkubwa wa kuwaleta watu wengi pamoja, kwa hiyo FIFA kumpa nafasi ya kushirikiana na Shakira katika wimbo rasmi wa Kombe la Dunia tayari wanajua uwezo wake ni upi.

Sema Burna Boy naye analipenda soka, mathalani mnamo Agosti 2024, alizindua akademi yake ya soka ‘Burna Boy Football Academy’ huko kwao Lagos, Nigeria.

Mradi huu unalenga kukuza na kuendeleza kizazi kijacho cha vipaji vya soka barani Afrika kupitia mpango wa mafunzo ulioandaliwa na wataalamu wa soka.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya akademi hiyo, mradi huo unalenga kusaidia makundi mawili ya vijana; kuanzia umri wa miaka minne hadi 15 na wale wenye umri wa miaka 16 hadi 21.

Burna Boy anafanya hayo yote baada ya muziki wake kupata mafanikio makubwa ambapo ametoa albamu saba hadi kufikia sasa.

Albamu hizo ni L.I.F.E (2013), On a Spaceship (2015), Outside (2018), African Giant (2019), Twice as Tall (2020), Love, Damini (2022), I Told Them… (2023), na No Sign of Weakness (2025).

Albamu yake, Twice as Tall (2020) alishinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Muziki Duniani 2021, na kumfanya Burna Boy kuwa msanii wa kwanza wa kiume Nigeria kushinda Grammy kupitia kazi yake binafsi.

Kabla ya Burna Boy, wasanii wa Nigeria kama Femi Kuti, King Sunny Ade, Babatunde Olatunji na Wizkid walikuwa wameshinda Grammy ila kupitia kazi walizoshirikishwa na wasanii wengine.

Ikumbukwe Burna Boy alianza kuvuma Afrika mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma, Like to Party kutoka kwenye albamu yake, L.I.F.E (Leaving ana Impact for Eternity) iliyokuja kutoka Agosti 12, 2013 na kuuza nakala 40,000 siku yake ya kwanza sokoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *