
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema itaendelea kuimarisha huduma za tiba ya magonjwa ya dharura na ajali pamoja na kuongeza wataalamu wa eneo hilo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haraka na salama zinazookoa maisha.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 29, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Magonjwa ya Dharura na Ajali yaliyofanyika Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa hospitali hiyo, Dk Yonazi Mbonea amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wataalamu wa tiba ya dharura katika kuokoa maisha ya wananchi.
Amesema kutokana na unyeti wa kazi hiyo, jamii bado inahitaji wataalamu hao kwa kiwango kikubwa ili kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za dharura za kitabibu.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na wataalamu wa tiba ya dharura na ajali katika kuokoa maisha ya wananchi. Kutokana na unyeti wa kazi yao, jamii bado inawahitaji kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za dharura za kitabibu,” amesema Dk Mbonea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura na Ajali MNH, Dk Juma Mfinanga amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hizo hospitalini hapo, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuokoa maisha ya wagonjwa.
Amesema vifo vya wagonjwa wa dharura vimepungua kwa zaidi ya asilimia 50 kutokana na kuimarika kwa huduma pamoja na mafunzo maalum yanayotolewa kwa wataalamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini.
“Tumeendelea kuimarisha uwezo wa kutoa huduma za haraka pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya kutoka maeneo mbalimbali nchini. Hatua hii imesaidia kusogeza huduma za dharura hadi katika zahanati na hospitali za wilaya,” amesema Dk Mfinanga.
Maadhimisho ya Siku ya Tiba ya Magonjwa ya Dharura na Ajali hufanyika kila mwaka Mei 27 kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa huduma za dharura katika kupunguza vifo na kuelimisha jamii kuhusu hatua za awali za huduma wakati wa dharura za kiafya.
Maadhimisho ya mwaka huu yamewakutanisha wataalamu wa afya kujadili maendeleo ya huduma za dharura nchini pamoja na changamoto zinazohitaji maboresho zaidi katika sekta hiyo.
