
Dar es Salaam. Waandishi wawili wa Mwananchi ni miongoni mwa washindi waliochukua tuzo katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat) kwa mwaka 2025.
Waandishi hao ni Julius Maricha ambaye ameshinda Tuzo ya Uandishi Bora wa Afya ya Uzazi na Devotha Kihwelo ameshinda Tuzo ya Babari Bora ya Utawala Bora 2025.
Pia Gazeti la Mwananchi limeshika nafasi ya tatu katika uandishi bora wa habari katika upande wa afya ya uzazi.
Nafasi ya kwanza katika kinyang’anyiro hicho imechukuliwa na Julius Maricha wa The Citizen huku The Guardian ikitajwa nafasi ya pili.
Tuzo hizo zimetolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo Mei 29, 2026 jijini Dar es Salaam huku zikishuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Jaji Nestor Kayobera ambaye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo.
Mshindi wa jumla katika tuzo hizo ametangazwa kuwa Simon Mkina kutoka Pambazuko Online na kukabidhiwa hundi ya Sh3 milioni na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera.
Kabla ya kuanza kutolewa kwa tuzo hizo, akizungumza na wanahabari, Jaji Kayobera amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kulinda haki, utawala bora na demokrasia ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisisitiza kuwa mahakama haiwezi kutoa haki bila ukweli, huku ukweli huo ukiutegemea uandishi wa habari wenye maadili.
Amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazowasaidia kushiriki katika maendeleo ya jamii na usimamizi wa haki.
“Mahakama haiwezi kutoa haki bila ukweli, na ukweli hauwezi kufika mahakamani bila mwandishi wa habari mwenye maadili. Waandishi wa habari si wageni katika ukumbi wa haki, ni mashahidi wakuu wa jamii na walinzi wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.
Alinukuu ibara ya sita ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayozitaka nchi wanachama kulinda misingi ya utawala bora, ikiwemo uhuru wa kujieleza, huku ibara ya saba ikisisitiza kuwa wananchi ndio msingi wa ushirikiano wa jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wake, wananchi hawawezi kushiriki kikamilifu katika maendeleo bila kupata habari sahihi na za kuaminika.
Katika hotuba yake, aliwataka waandishi wa habari kuzingatia kanuni tatu muhimu za uandishi bora ambazo ni ukweli uliothibitishwa, maslahi ya umma na kulinda utu wa binadamu.
Amesema kama ilivyo mahakamani ambapo anayetoa madai hutakiwa kuthibitisha, ndivyo ilivyo kwa mwandishi wa habari anayetakiwa kuhakikisha taarifa anazochapisha zimethibitishwa.
Aidha, alieleza kuwa sekta ya habari ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuenea kwa habari za uongo, pamoja na changamoto mpya zinazoletwa na teknolojia na akili mnemba.
Amesisitiza kuwa changamoto hizo zinahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, taasisi za habari na vyombo vya kujidhibiti ili kuimarisha taaluma ya habari na kulinda maadili ya kazi hiyo.
Aliwataka waandishi wa habari vijana kuendelea kulinda misingi ya taaluma hiyo na kutunza heshima ya vyombo vya habari vilivyojengwa kwa juhudi za watangulizi wao.
