
Dar es Salaam. Inaelezwa kuwa baadhi ya wasichana hujikuta wakikosa masomo kwa siku tatu hadi saba kila mwezi wanapokuwa kwenye hedhi kwa sababu ya kukosa taulo za kike ‘pedi’.
Wasichana hao hulazimika kubaki nyumbani wakihofia kuchafuka na kuaibika mbele za watu.
Hayo yameelezwa leo Mei 28, 2025 na Mwenyekiti wa Taasisi ya Afya na Tumaini Endelevu (ATE), Lilian Lema wakati wa ziara ya taasisi hiyo katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko kutoa elimu ya afya ya hedhi kwa wasichana.
Hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya hedhi salama duniani iliyoambatana na ugawaji wa taulo za kike.
Akizungumza na wanafunzi wa kike katika shule hiyo Lilian amesema upatikanaji wa uhakika wa pedi katika shule za msingi na sekondari nchini utaimarisha elimu ya mtoto wa kike.
“Mtoto wa kike anapokuwa na uhakika wa kupata vifaa vya kujihifadhi anapokuwa katika siku zake inampa amani ya kujifunza na kuzingatia masomo yake bila ya kuwa na wasiwasi wa kuchafuka,”amesema Lilian.
Katika hatua nyingine Lilian amewaasa wasichana kujitunza na kuzingatia usafi haswa wanapokuwa katika siku za hedhi.
Pia pale wanapokumbana na hali isiyo ya kawaida wakati hedhi ikiwemo maumivu makali ya tumbo kutokwa na damu nyingi au zaidi ya siku saba kutoa taarifa kwa wazazi, walezi au walimu ili waweze kupatiwa msaada.
“Mkishafikia hatua hii ya kuanza kupata hedhi hakikisheni mnajitunza na kuniweka mbali na vishawishi vyote vitakavyowaweka katika hatari ya kupata ujauzito,”amesisitiza Lilian.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Ajrath Kashakara amesema pedi h amewataka wadau waendelee kutoa elimu kuhusu masuala ya hedhi salama na umuhimu wa elimu ili kuendelea kubadilisha maisha ya wasichana na jamii ya kitanzania kwa ujumla.
Nae mwanafunzi Mariam Shabani amesema taulo hizo zitawafanya kujiamini na kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kitaaluma na michezo hata katika kipindi cha hedhi.
Pia elimu waliyoipata itawasaidia kujitunza na kuwa salama wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
Kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mwaka 2023 unabainisha kuwa asilimia 60 ya wasichana wanashindwa kumudu gharama za ununuzi wa taulo za kike ambazo ni bidhaa muhimu katika maisha ya mtoto wa kike.
