Wizara ya Afya ya Uganda imethibitisha visa sita vipya vya ugonjwa wa Ebola, na hivyo kufanya jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa nchini humo kufikia 15.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, wizara hiyo ilisema kuwa visa vipya viligunduliwa miongoni mwa watu waliokuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa awali kuwa na Ebola.
Uganda ilirekodi kisa chake cha kwanza cha Ebola tarehe 15 Mei baada ya kifo cha raia wa DRC ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali binafsi. Tangu wakati huo, visa vingine vya maambukizi vimeripotiwa, ikiwemo kwa baadhi ya wahudumu wa afya.
Wizara ya Afya pia imetangaza kuwa kwa sasa inafuatilia watu 668 waliowahi kuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola, kama sehemu ya juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo. Wakati huohuo, wagonjwa wawili wa Ebola wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupona kabisa ugonjwa wa virusi vya Ebola.
Katika maendeleo yanayohusiana na afya ya umma, Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kukabiliana na Majanga ya Magonjwa cha Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC).
Kituo hicho kitafanya kazi kama kitovu cha kikanda cha ufuatiliaji wa magonjwa, uratibu wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, msaada wa maabara, maandalizi ya dharura, utafiti, pamoja na kupeleka wataalamu wa afya wakati wa dharura za afya ya umma na milipuko ya magonjwa.
#chanzobbcswahili

(Feed generated with FetchRSS)