Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imesaini makubaliano ya ushirikiano na Shirikisho la Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Norway (NAD) yenye thamani ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kuimarisha elimu jumuishi kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo leo Jumapili Juni 14, 2026, Mjini Unguja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdulla Said amesema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka wa kuleta mabadiliko chanya, hususan katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu katika elimu zinatekelezwa kikamilifu.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) tayari imeweka sera na maboresho mbalimbali ya elimu inayolenga kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata elimu bila vikwazo.
“Huu ni msaada mkubwa na hatua ya kupongezwa. Nina imani kwamba baada ya miaka mitano Zanzibar itakuwa imepiga hatua kubwa katika elimu jumuishi,” amesema Khamis.
Amebainisha kuwa, mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha lugha ya alama inafundishwa kama somo katika shule zote, kama zilivyo lugha nyingine ili kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Pia, amesema Serikali inalenga kuwa na walimu wote wenye uelewa wa elimu jumuishi ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanajumuishwa kikamilifu katika shule zote bila kukabiliwa na upungufu wa wataalamu.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (kulia) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi mkaazi wa Norwegian Association of Disabled-NAD, Abdulla Amour baada ya kumaliza kusaini hati ya makubaliano kushirikiana katkka kuimarisha elimu mjumuisho Zanzibar.
“Sasa hivi tumeajiri walimu 90 wa elimu jumuishi, lakini dhamira yetu ni kuhakikisha walimu wote wanapata mafunzo haya ili wanafunzi wote waweze kujumuishwa kwa usawa,” amesema.
Khamis amesema maeneo mengine yatakayofaidika na makubaliano hayo ni ya utekelezaji wa sera na mikakati ya elimu jumuishi pamoja na kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu visiwani Zanzibar.
Akitaja sababu ya ushirikiano huo ambao pia utahusisha kujenga uwezo kwa maofisa wa wizara waweze kusimamia ipasavyo programu za elimu jumuishi.
Amesema NAD inatekeleza miradi mingi visiwani humo kwa zaidi ya miaka tisa, ikiwa na uwekezaji unaokadiriwa kufikia zaidi ya Sh5 bilioni katika sekta mbalimbali za ulemavu na elimu jumuishi.
Khamis amesema jitihada hizo zimesaidia kuongeza uandikishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu katika shule za serikali na binafsi, ambapo zaidi ya wanafunzi 1,000 wamenufaika.
Amesema kupitia ushirikiano huo kumekuwa na uandaaji wa miongozo ya kufundishia walimu kuhusu elimu jumuishi, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa na kuboresha utekelezaji wa sera.
Mkurugenzi Mkazi wa NAD, Abdulla Amour amesema shirika hilo limejikita katika kukuza haki za watu wenye ulemavu kupitia elimu mjumuish, uchechemuzi wa sera na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema makubaliano hayo ni mwendelezo wa ushirikiano ulioanza mwaka 2019, akibainisha kuwa lengo ni kuimarisha mfumo wa elimu kuwa jumuishi zaidi.
“Tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu katika kubadilisha mfumo wa elimu kuwa jumuishi. Haya makubaliano ni hatua ya kurasimisha kazi ambayo tayari imekuwa ikiendelea,” amesema.
Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mohamed Nassor Karim amesema pande zote mbili zimejizatiti kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano hayo unaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, hususan elimu jumuishi.