Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuchangamkia fursa za miradi ya hewa ya ukaa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na miradi ya maendeleo na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Sendiga ametoa wito huo leo Alhamisi Juni 25, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Orkesumet, ambapo pia alizindua basi lililonunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, samani mpya za ukumbi wa mikutano na kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024/25 iliyoipa Halmashauri ya Simanjiro hati safi.
Akizungumza katika kikao hicho, Sendiga amesema miradi ya hewa ya ukaa imeleta manufaa makubwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo. Picha na Joseph Lyimo.
“Wenzenu wa Wilaya ya Kiteto wamefaidika kwa kiasi kikubwa kupitia miradi ya hewa ya ukaa kwa kupata miradi mbalimbali ya maendeleo. Nanyi mnapaswa kuchangamkia fursa hii kwa manufaa ya wananchi wa Simanjiro,” amesema Sendiga.
Amesema miradi hiyo inaweza kusaidia upatikanaji wa fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa shule na huduma nyingine muhimu kwa jamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleya Mollel amesema halmashauri imepokea maelekezo hayo na ipo tayari kuyafanyia kazi. Amesema miradi hiyo ina mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi.
Baadhi ya wakazi wa Simanjiro wameunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo, akiwamo Esupati John ambaye amesema miradi ya hewa ya ukaa ni fursa muhimu kwa kuwa inaleta fedha za maendeleo huku ikichangia uhifadhi wa mazingira.
Naye Aloyce Balthazar amesema jamii za wafugaji katika wilaya za Kiteto na Longido tayari zimeanza kunufaika na miradi hiyo, hivyo wananchi wa Simanjiro wanapaswa kuunga mkono utekelezaji wake. Ameongeza kuwa elimu zaidi inahitajika ili kuondoa hofu zilizopo kuhusu miradi hiyo na kuwawezesha wananchi kuelewa manufaa yake.