
Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere aliwahi kusema tusitatue matatizo yetu kwa kujifanya hayapo, nami nimewiwa kuazima usemi huo kwamba yapo mambo yakifanyika, njia ya maridhiano ya kisiasa na kijamii tunayoitamani ni nyeupe.
Wahenga wanasema siku zote ukweli una sifa moja tu kwamba hata ukiukataa, kamwe hauwezi kugeuka kuwa uongo na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, nami nimeamua kuusema ukweli huo ili Taifa letu lipone na tufungue ukurasa mpya.
Hakuna ubishi kuwa matukio ya ghasia za Oktoba 29,2025 na siku zilizofuata yamejeruhi mioyo ya Watanzania na kuliingiza Taifa letu katika roho ya chuki na visasi na tusiposema ukweli, hakika dhambi hii itatutafuna hadi tunaingia kaburini.
Jambo la kwanza ambalo Serikali na viongozi wetu wanatakiwa kulifanya ni kukiri tu na kuomba radhi kwa yaliyotokea na kusababisha vifo vya Watanzania wenzetu 518 na majeruhi zaidi ya 2,000, ambao hawakustahili kuuawa au kujeruhiwa.
Simulizi zinazotia uchungu za baadhi ya mashuhuda ni kwamba wapo watanzania waliouawa au kujeruhiwa kwa risasi ambao hawakuwa katika ghasia zile, bali waliuawa majumbani mwao au barabarani wakati wakirudi majumbani mwao.
Sio wote waliuawa katika vurugu zile hivyo si sahihi kuwachanganya wote katika kapu moja, na hiki ndicho ambacho kinaumiza watanzania walio wengi na hata kama wapo alikuwa wakiandamana ili kupindua Serikali, walistahili kuuawa?
Jambo la pili, ni kwa Serikali kufanya kila linalowezekana juu ya uwezo wake kufuta kesi zote za kisiasa ikiwamo ya mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Tundu Lissu na kesi zilizotokana na ghasia zile ili sasa tufungue milango ya kuridhiana kama taifa.
Ninavyo mimi, kesi hii ya Lissu inachangia kuchochea chuki kwenye jamii kutokana na aina yenyewe ya mashitaka na ushahidi ambao tayari upo kwenye uwanja wa umma (public dormain), ambao sitauzungumzia katika makala haya ya leo.
Wala sio mimi pekee na baadhi ya watanzania tunaona Lissu anastahili kuachiwa huru, kwani hata Jumuiya za Kimataifa kama Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Ulaya (EU) na hata taifa kubwa kama Marekani nalo limetoa wito wa kuachiwa kwake.
Tufanye haya kwa masilahi mapana ya nchi yetu na wala si madhaifu kumuachia.
Kama kuna ulazima wa kumshitaki Lissu kwa matamshi yale basi tumshtaki chini ya kifungu 390 cha Kanuni ya Adhabu Urekebu wa mwaka 2023 kinachoeleza kuwa mtu yeyote anayemshawishi au kumchochea mtu mwingine kutenda kosa anakuwa na hatia ya uhalifu na anaweza kushtakiwa kama mkosaji mkuu.
Lakini kama tutaamua kumshtaki kwa kosa hilo, basi hata wale wa upande wa pili waliotoa matamshi ya uchochezi kama mshindi hapatikani kwenye sanduku la kura au walishiriki kuua watu huko porini nao washtakiwe kwa uchochezi.
Jambo la tatu ambalo Serikali inapaswa kulifanya ni kulipa fidia familia zilizopoteza wapendwa wao na hii ijumuishe familia ambazo wapendwa wao wamepotezwa lakini iende mbali zaidi na kuwalipa fidia wale wote waliojeruhiwa.
Fidia hizi ziwajumuishe pia zile familia ambazo zinatafuta miili ya ndugu zao.
Hatutakuwa Taifa la kwanza kufanya haya kwa masilahi mapana ya nchi yetu kwani mwezi uliopita, majirani zetu Kenya wametenga Sh40.6 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia waathirika wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.
Ukiukwaji huo ulitokana na maandamano ya mwaka 2017 na 2022 ambayo yalihusishwa na migogoro iliyotokana na uchaguzi mkuu, maandamano ya kupinga muswada wa fedha wa mwaka 2024 na maandamano ya sabasaba ya 2025.
Jambo la nne ni kwa Serikali kutangaza kuwachukulia hatua maofisa wa vyombo vya dola, ambao watathibitika walitumia nguvu kupita kiasi kuzima ghasia hata kama walikuwa wanatekeleza amri halali, lakini ni lazima iwe ndani ya sheria.
Ninafahamu Rais Samia ameunda Tume kuchunguza jinai katika vurugu zile, ni jambo jema sana ila tutaongeza tatizo zaidi endapo wananchi wataona kuna watu fulani fulani tu ndio wanaolengwa na sio wale wao wanaodhani ndio walengwa.
Baada ya kufanya yote hayo, Rais sasa kwa mamlaka aliyonayo, auende Tume ya Upatanishi na Maridhiano ili kulileta pamoja Taifa na Tume hiyo iundwe na watu wanaoaminika na kukubalika katika jamii ili tulijenge upya Taifa letu.
Katika kuingia katika meza ya mazungumzo ili kuelekea katika maridhiano, ni muhimu sana ukweli ukatawala ili kujua nani amemkosea nani, kwenye nini na ili tusirudi tulikotoka tufanyeje, lakini kila upande ukishikilia lake, hatutoboi.
CCM na Serikali yake ni lazima wakubali kujishusha na kupoteza sehemu ya misimamo yao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nao wajishushe na vivyo hivyo kwa wadau wote wa amani.
Sote tunafahamu kwa nini mchakato wa Katiba mpya ulifeli, kwa hiyo CCM ni lazima kiwe na dhamira ya dhati ya kulitoa Taifa letu katika mkwamo huu wa kisiasa, Chadema vilevile watambue hilo na watanzania wote tutambue hilo.
Lakini jambo la mwisho muhimu sana, ni kwa viongozi wetu kujiepusha na kauli ambazo zinazoamsha hisia za hasira na kutonesha vidonda kwa waliopoteza wapendwa wao au kupata vilema kutokana na ghasia zile za Oktoba 29, 2025.
Mambo hayo matano yaende sambamba na kutatua changamoto zilizotufikisha katika ghasia zile za Oktoba 29, 2025 kama ambavyo zimeelezwa na Tume aliyoiunda Rais Samia Suluhu Hassan chini ya Jaji mkuu mstaafu Othman Chande.
Tume hiyo ilisema ghasia na maandamano yale yalitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa, kwa hiyo hatuna sababu ya kutafuta mchawi wakati mchawi tunamjua.
Miongoni mwa changamoto hizo ni madai ya Katiba mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.
Zingine ni masuala ya kiuchumi yanayojumuisha ugumu wa maisha, kukosekana kwa usawa katika fursa za ajira na za kiuchumi, mazingira ya biashara na uwekezaji yasiyo rafiki, utitiri wa kodi na tozo na mfumo usio rafiki wa kodi.
Tume ikataja changamoto nyingine kuwa ni masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na madai ya utekaji wa watu, mauaji na kupotea au kupotezwa kwa watu hapa Tanzania.
Binafsi ninaamini changamoto hizo zipo ndani ya uwezo wetu kama kutakuwa na utashi wa kisiasa, lakini tukiendelea na hali hii ya ‘state of denial’ (kutokubali ukweli), nchi hii itapitia hekaheka na misukosuko pengine hadi 2030 au zaidi.
Ni ukweli mchungu lakini hatuna budi kuusema ili kuliponya Taifa letu kwa sababu tukiendelea na hii ‘state of denial’ na kutafuta mchawi wakati mchawi wetu tunamjua na Jaji Chande na Tume yake wametueleza bayana, basi hatutatoboa.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900