Meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, amemtaja Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuwa ni mhalifu wa kivita, na kuitaka serikali ya Marekani kutekeleza hati ya kukamatwa kwake iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iwapo atatia mguu katika ardhi ya Marekani.

Mamdani amesisitiza katika ujumbe wa video uliopakiwa kwenye jukwaa la X kwamba: “Benjamin Netanyahu ni mhalifu wa kivita, msanifu mkuu wa mauaji ya halaiki ya kutisha dhidi ya watu wa Palestina.”

Amesema kuwa Netanyahu anawajibika moja kwa moja kwa maangamizi ya zaidi ya Wapalestina 73,000, kulenga makusudi hospitali, na kuzuia upatikanaji wa chakula na misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wanaoteseka katika Ukanda wa Gaza.

Ni vyema kukumbusha kuwa ICC ilitoa hati za kukamatwa mnamo Novemba 2024 kwa Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita wa utawala huo, Yoav Gallant, kutokana na  uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vita vya Gaza.

Mamdani ameonya kuwa Marekani ina sehemu kubwa ya dhima katika jinai hizi, akisema, “Sisi, kama Wamarekani, tunafadhili mabomu yanayotekeleza mauaji haya.”

Ameongeza kwa msisitizo kwamba: “Kuna sababu ya msingi iliyoifanya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutoa hati ya kukamatwa kwake. Mtu yeyote anayetumia macho yake, mwenye moyo, na mwenye dhamira timamu, anapaswa kutambua uharibifu mkubwa aliouleta na kuelewa vyema kuwa anastahili kufikishwa mbele ya sheria.”

Ingawa Mamdani alikiri kuwa serikali yake jijini New York haina mamlaka ya kisheria ya kutekeleza hati hiyo peke yake, ametoa wito wa wazi kwa mamlaka za ngazi ya juu nchini humo kutekeleza amri ya ICC. “Serikali ya shirikisho, hata hivyo, inayo mamlaka hayo, na ninawatolea wito wajiunge na ICC na kutekeleza hati hii. Na natamka wazi bila kuficha kwamba: Benjamin Netanyahu hakubaliki katika Jiji la New York, wala mhalifu mwingine yeyote wa kivita anayetembea huru.”

Kauli hii inakuja huku kukiwa na mgongano wa kimaslahi, ambapo Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema Jumatatu kuwa Netanyahu “hatakamatwa, kwa namna yoyote ile, akiwa nchini Marekani.” Msimamo huu wa Washington unaendelea kuthibitisha uungaji mkono wake wa moja kwa moja kwa jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ubinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *