Dar es Salaam. Miaka kadhaa iliyopita. JPM akiwa hai na kuzilaza mbavu zake pale Magogoni. Dar es Salaam ikiwa chini ya Paul Christian Makonda. Bunge likimilikiwa na joho la Job Ndugai na Diamond akiwa katika penzi la Zari. 

Ben Pol na Moyo Mashine. Of coz Jux akinata na huba la Vannessa. Achana na Konde Boy aliyekuwa penzini kwa Sarah wa Mzungu. Huku Irene Uwoya na Dogo Janja wakiunganisha yale maeneo yao nyeti kwa ndoa ya Kichina.

Nipo Mlimani City, hata sikumbuki nilifuata nini. Sikuwa na njaa njaa za kipimbi. Nilikuwa safi ile safi kinoma, sikuwa tofauti na wakazi wa New York, Paris, Bangkok ama London Town. Mtamu kweli kweli lakini mpweke kinoma.

Upweke wangu ulipelekea nipate adha ya shingo. Niligeukageuka mithili ya feni kuangazia pisi kali zilizotua kwa kupokezana. Kuna maeneo ya mkusanyiko ya watu yenye warembo kuzidi Mlimani City? Ndiyo inawezekana.

Mwenge, Posta, Ferry, Airport, Sinza hadi Mtoni kwa Aziz Ally. Kuna ‘pisi kali’, ila zinakosa kitu cha kuitwa ‘kwalite’. Mlimani zipo pisi za kutoka maeneo hayo hayo, lakini zikifika pale zinabadilika kwa kila kitu.

Kwanza uvaaji, pili utembeaji na tatu uongeaji. Kimsingi watu wa maeneo ya Mlimani City, Dar Free Market na maeneo ya dizaini hiyo. Wengi wao ni feki na siyo halisi, ufeki ni mwingi kuliko uhalisia. Wanajipa umuhimu sana. 

Katika kuzungusha zungusha hili bichwa langu. Ghafla nikamuona kiumbe wa Mola Mwenyezi, uzao wa Magdalena. Toto flan ambaye sikuhitaji ‘vieiara’ kuujua ule ubora wake. Kuanzia sura, shepu, rangi, ngozi, mavazi hadi macho.

Alikuwa anatokea ndani ya moja ya maduka yaliyojaa Mlimani City pale. Kuna pisi mnakutana kwa mara ya kwanza, siku hiyo hiyo na ndoa inatangazwa. Hutaki kusikia la muadhini wala mnadi swala, ni mwendo wa mshenga na mahari.

Ndo huyu sasa, alikuwa na sifa zote za mamtu. Siku hizi mambo ya tabia njema yamepitwa sana. Ni upuuzi kuoa mtu kwa sababu ya tabia yake, ukaacha kutazama wezere na macho ya kurembuliwa na lile deko flan la kike. 

‘Blaza’ mimi sioi tabia, simtafuti katekista ama shemasi. Nataka pisi ya kupamba sebule yangu na chumba changu. Nataka mtoto wa kupendezesha mtoko wangu mbele ya washikaji. Nataka kuoa pambo siyo chombo.

Jiheshimu mjomba. Tabia njema  kuna maeneo mengi ya kupeleka. Katika ndoa yangu lete pisi ndefu sampuli ya Beyonce, Alicia Keys au Posh. Posh wa Beckham siyo ‘eksi’ wa Mmakonde, ingawa hata yeye pia ni mali safi. Ndiyo!

Mtoto akashusha guu mmoja kwa ngazi. Akapozi, pozi la picha za ‘kava’ la ‘magazini’ au filamu zile za vituzi kutoka kule Hollywood. Akageuka. Akili zikajirudi rasmi na kugundua siyo ndoto nionacho mbele yangu bali ni kweli.

Nipo laivu Mlimani City. Na mbele yangu namuona msichana mzuri. Ambaye katoka ndani ya Mlimani City akielekea kwenye maegesho ya magari. Lakini ghafla alizubalia jambo akilitazama kimshangao na hamu kubwa upande wa pili.

Kupikicha macho nagundua kuwa si yeye tu. Kuna pisi kadhaa zipo ‘araundi’ pale, zote macho yako kulekule. Ndani ya dakika kadhaa yule dem akatoweka usoni pangu kutokana na wingi wa jinsi yake kuongezeka.

Kuna nini? Nilijiuliza huku nikiinua uso kutaka umbea. Yaani nilileta uswahili kidogo, na unajua kwetu uswahili ni sunna. Kutazama hivi, kumbe kuna msanii anapita mitaa ile, ndiye aliyeyahamisha macho ya warembo wote. Msanii gani? 

Ndo kwanza anatokatoka kisanii hana hata nyimbo tano. Siwezi kukumbuka mwaka ‘ekzaktili’ ila naweza kuelezea mazingira yake. Ni wakati ule Lissu akihamishiwa kutoka hospitali ya pale Nairobi na kupelekwa Ubelgiji. 

Nyakati zile Clatus Chotta Chama ndo anatua Msimbazi. Ni mpya mpya, huku Yanga wakipambana na kiwango cha Moringa na Ykpe. Msanii gani huyu anapapatikiwa hivi na madem? Mondi? Alikiba? Konde ama Rich Mavoko?

Nyakati hizo msanii kutamba nje ya WCB ni dhambi. Waliotamba ni wachache kama Alikiba, Darassa, Ben Pol na Peter Msechu kidogo. Naye kwa sababu ya nyimbo zake za matukio. Nje ya hapo ni WCB tu ndiyo waliotamba kila kona.

Akili ya haraka haraka ikanituma WCB. Pengine Mondi katimba na ‘kruu’ yake. Maana Mondi yule wa moto, halafu bado ana ‘utineja’ wa kutaka kukera watu tu. Lakini siyo watu wa WCB, siyo Kiba, Ben Pol wala Darassa. Ni nani huyu sasa?

Marioo. Dogo ndo anachomoka chomoka na pini zake mbili tatu. Kuamini kwamba anaweza peke yake kukusanya msitu wa watu pale Mlimani City ni ngumu sana. Haswa hulka ya watu wanaojoin mitaa ile, lakini dogo aliweza.

Ingekuwa uswahilini siyo kesi. Huko hata ugomvi wa baba na bintiye hukusanya msitu wa watu. Uswazi hata vita ya majogoo au mbwa hubeba nyomi la watu tena wakubwa kwa watoto. Uswazi ni kwere na hawana dogo.

Lakini huyu dogo alikusanya pisi kali zile za shopping Mlimani City. Pisi za kucha ndefu, nyusi ndefu, nywele ndefu. Lakini sketi zao ni fupi, hata blauzi zao pia ni fupi na ukiwatongoza pia jibu fupi. Wale madem wa macho matatu bila ni zaidi ya ndoa.

Ilinishangaza kidogo kwa sababu moja tu. Kwamba msanii mpya halafu anakimbiza nje ya WCB? Ile WCB ya Mondi, Fella, Tale na Sallam. Ilikuwa timu kubwa kama Barcelona ya Iniesta, Xaiv ‘Ageini’, Messi, Peque, Busqueti na Puyol.

Marioo  alitoboa katikati ya msitu wa Konde Boy, Rich Mavoko, Van Boy, Lavalava, Mbosso na Mondi akiwapa ‘bakapu’. Wakati huo pia Aslay wa moto, Kiba, Ben Pol na wengineo. Lakini Marioo kivyake akapasua anga la muziki. Mama Aminaaa.

Kuna namna watu tunachukulia vitu poa. Marioo alichomoza kwenye muziki katikati ya vita ya kuikuza WCB, ili iwe himaya ya kibabe. Msanii kutoka kisanii nje ya WCB, ilikupasa uwe ‘ekstra odinare’. Sasa ndo Marioo.

Kama utani tu Marioo akawa juu ya Mbosso na Lavalava. Kabla ya ‘kambaki’ ya Mbosso juzi kati. Ni ukweli kwamba Marioo alitoka kisanii na akawa mkubwa nje ya mipaka ya ‘Warumi’ wa WCB na ‘Herode’ wao Mondi. 

Wengi walishindwa. ‘Imejini’ wapo walioshindwa wakiwa mule mule ndani ya WCB. Leo Marioo yupo eneo moja na wakubwa wengine kisanii. ‘Akipushi’ mikoko mikali na kumiliki mtoto mzuri Paula. Yupo kwenye dunia yake. 
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *