Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mafuta ghafi yatakayopita katika Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania yataanza kusafirishwa kwenda sokoni ifikapo Julai, mwaka huu.

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumamosi Februari 7, 2026 wakati wa ziara ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na kujadiliana masuala kadhaa ukiwamo mradi wa EACOP.

Rais Museveni amewasili nchini leo Februari 7, 2026 kwa ziara ya kikazi ya siku moja na amefanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Rais Samia, Ikulu jijini Dar es Salaam, kabla ya kukutana na timu zao za mawaziri na baadaye kuzungumza na vyombo vya habari.

Ziara ya Museveni ni ya kwanza kwa kiongozi wa kimataifa kuitembelea Tanzania tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na Rais Samia kushinda uchaguzi huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo ya pamoja na ujumbe wa Uganda uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam  leo Ijumaa Februari 7, 2026.

Vilevile, ziara hiyo ni ya kwanza kwa Museveni tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika Januari 15, 2026, akichaguliwa kwa muhula wake wa saba tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.

Wakizungumza na vyombo vya habari, viongozi hao wameeleza mambo waliyoyajadili kwenye mazungumzo yao ya faragha na baada ya kukutana na timu zao za mawaziri huku waliangazia masuala mtambuka.

Rais Samia amesema timu za mawaziri na wasaidizi wao zilikutana wakati wao wakifanya mazungumzo ya faragha na kwamba miongoni mwa mambo waliyojadili ni ujenzi wa mabomba ya nishati.

Mbali na bomba la kusafirisha mafuta ghafi la EACOP, amesema wamejadili pia kuhusu bomba la gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda na bomba la mafuta safi kutoka Uganda kwenda Tanga.

“Tunamshukuru Mungu kwa mazungumzo yetu, huenda meli ya kwanza ikaondoka Tanga kwenda pale mafuta yanakopelekwa. Ndani yake kuna mambo mengine tunayafanyia kazi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa wamejadiliana pia kuhusu bandari kwa kuwa Tanzania inategemewa na nchi ambazo hazina bahari, hivyo wamejadiliana namna watakavyozitumia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Februari 7, 2026.

Kwa upande wa reli, amesema wamewaeleza wenzao wa Uganda kuhusu mradi wa reli kutoka Tanga hadi Musoma na huko wataweza kuunganisha kwa meli hadi Uganda.

Pia, amesema wamewaeleza kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ya Isaka hadi Rusaunga na kwamba wameiomba Uganda nayo ipokee ujenzi wa reli hiyo hadi Murongo kwa upande wa Uganda.

“Tumekuwa tukiondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kikodi. Kwa jumla biashara kati yetu imekua sana, isipokuwa kuwa vikwazo vidogo vidogo ambavyo mara nyingi vinasababishwa na watendaji,” amesema Rais Samia.

Mbali na masuala hayo, Rais Samia amemshukuru Rais Museveni kwa kuwa, mwaka jana Tanzania na Uganda zilikuwa zinawania nafasi ya uwakilishi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki, hata hivyo Museveni alijitoa ili kutoa nafasi kwa Tanzania kwenye nafasi hiyo.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni pamoja na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Februari 7, 2026.

“Uganda nayo inagombea nafasi kama hiyo kwenye Umoja wa Afrika (AU), nasi tunaahidi tutawapa nguvu katika hilo,” amesema Rais Samia kwenye mkutano huko na vyombo vya habari.

Kwa upande wake, Rais Museveni amesema katika mazungumzo na mwenyeji wake, amesisitiza umuhimu wa kurejea kwenye madhumuni ya ukombozi wa Afrika ambayo yalikuwa na malengo matatu; kupata uhuru, kuwaletea wananchi maendeleo (kuzalisha bidhaa na huduma) na usalama wa kimkakati (kujihami).

“Baada ya uhuru, tunahitaji kuunganisha nguvu zetu, kuna vitisho vinajidhihirisha katika kanda yetu, hivyo ni muhimu tukashirikiana katika hilo,” amesema Rais Museveni.

Akirejea Azimio la Kampala la mwaka 1965, Rais Museveni amesema walikubaliana kwamba Tanzania itazalisha matairi, Uganda itazalisha nguo (textile) na Kenya ikizalisha kitu kingine.

“Tunahitaji kurejea kwenye muundo kama huu uliovurugika, sijui nini kilitokea,” amesema Rais Museveni akisisitiza ushirikiano wa kikanda ili kujihami na vitisho vya kiusalama lakini pia kuimarisha uchumi wao.

Kiongozi huyo wa Uganda ameonya wananchi katika ukanda huu wasiwe kama machifu wa zamani walioona matishio ya Wazungu kuja Afrika lakini hawakuchukua tahadhari zozote za kujihami kiusalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *