Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Kongamano la Usalama la Munich ambalo kwa kawaida huzingatiwa kuwa tukio muhimu na lenye hadhi kubwa, limegeuka kuwa “sarakasi ya Munich” kuhusu masuala ya Iran.

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Iran, ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba: “Inaonekana kuwa Umoja wa Ulaya umechanganyikiwa. Chanzo cha kuchanganyikiwa huku ni Ulaya kutokuwa na uwezo wa kuelewa vizuri matukio yanayotokea ndani ya Iran. Mwelekeo jumla wa Ulaya ni hatari na unatia wasiwasi.”

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa: “Kwa mtazamo wa kistratijia, Umoja wa Ulaya usio na malengo umepoteza uzito wake wote wa kijiopolitiki katika eneo. Ni wazi kuwa Ujerumani inaoongoza katika kukabidhi kikamilifu sera zake za kieneo kwa utawala wa Israel.”

Araghchi ameandika zaidi kwamba kupooza na kutokuwa na umuhimu kwa Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya kunaonekana wazi katika matukio yanayohusiana na mazungumzo ya sasa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amebainisha kuwa: Ulaya, ambayo zamani ilikuwa moja ya pande kuu katika mazungumzo, sasa haionekani popote. Kwa upande mwingine, marafiki wa Iran katika eneo sasa wana nafasi zaidi kuliko Troika hii dhaifu na iliyotengwa ya Ulaya.

Kongamano la 62 la Usalama la Munich linafanyika nchini Ujerumani, katika hali ambayo Umoja wa Ulaya na wakuu wa serikali za Magharibi wanaitegemea sana Marekani katika kutekeleza matakwa na mipango yao.

Umoja wa Ulaya, hasa baada ya kuanza vita vya Ukraine, umekuwa tegemezi zaidi kwa mwavuli wa usalama wa Marekani katika uwanja wa ulinzi na usalama kuliko wakati mwingine wowote. Utegemezi huu unazifanya sera za Brussels katika masuala muhimu kama vile Iran kutekelezwa kwa msingi wa matakwa ya Washington, hata kama sera hizi zinakinzana wazi wazi na maslahi ya kiuchumi au kidiplomasia ya Ulaya.

Lobi zenye mfungamano na utawala wa Kizayuni katika nchi za Ulaya hususan Ujerumani nazo zina nafasi muhimu katika uundaji wa sera za Ikulu ya White House dhidi ya Iran.

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Kwa mtazamo wa Iran na wachambuzi wengi wa kujitegemea, Ulaya si tena mchezaji mwenye “misingi thabiti”, bali imekuwa wakala wa kisiasa wa Washington na Tel Aviv, na kwa sababu hiyo imepoteza uwezo wa kuzungumza na wachezaji wengine huru, hususan Iran, na hivyo kushindwa kudiri matukio ya ndani na kieneo.

Katika ngazi ya kikanda na kimataifa, dunia inahama kutoka mfumo wa kambi moja yenye nguvu inayoongozwa na Marekani kuelekea mfumo wa pande nyingi zenye nguvu. Ulaya imepoteza ufumbuzi wake wa kijiopolitiki na hivyo kuzipa nchi za eneo, zikiwemo Iran, Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na Misri, fursa ya kuwa maamuzi wakuu katika matukio ya eneo.

Katika ngazi ya kimataifa, China, Russia, Iran, India na Brazil zimeunda muungano mpya wa kiuchumi na kifedha, katika hali ambayo Ulaya inashughulishwa na mgogoro wa nishati na kiuchumi na kuongezeka kwa makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na hivyo kupoteza uwezo wake wa ushawishi katika ngazi ya kimataifa.

Kwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, Kundi la BRICS na kusaini makubaliano ya pande mbili na Russia, China na nchi za Ghuba ya Uajemi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepanua uhusiano wake wa kimataifa na kieneo na hivyo kufanikiwa kubuni upeo mpya katika siasa za nje.

Mbinu hii mpya ya Iran imesimama kwenye msingi wa “usalama wa kikanda bila utegemezi”, ambayo inazichukulia nchi jirani sio kama tishio, bali kama washirika wema katika kudhamini usalama wa eneo. Wakati mchezaji kama vile Umoja wa Ulaya anapopoteza uhuru wake wa kimkakati, huwa hatafuti tena amani, bali hutaka kuonyesha jinsi alivyo mwaminifu kwa mchezaji mkuu, yaani Marekani.

Suala hili hupelekea makongamano kama vile ya Munich, badala ya kuwa mahali pa mijadala muhimu na yenye kujenga, kuwa jukwaa la maneno na matamshi matupu yasiyotekelezeka kivitendo, na kwa mtazamo wa Iran, yanakuwa tu maonyesho ya burudani na sarakasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *