
Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wamevamia tena Msikiti mtakatifu wa Al-Aqswa na kufanya vitendo vya kichochezi dhidi ya kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.
Uvamizi huo ulifanyika jana ambapo huko Palestina ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ripoti zinasema makumi ya walowezi wa Kizayuni jana walivamia Msikiti wa al-Aqswa, na sambamba na kupiga nara dhidi ya Wapalestina, walifanya vitendo vya kichochezi katika eneo hilo takatifu.
Msikiti wa al-Aqswa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds, na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo; lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.
Walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali mara kwa mara wamekuwa wakivamia Msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na askari usalama wa utawala haramu wa Israel.
Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.