Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Marekani imeitoa kafara kila nchi kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi hazizipi ulinzi nchi wenyeji.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: Vita hivi (vya kutwishwa vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran) vimethibitisha wazi jambo moja; Kambi za Marekani katika eneo hazimlindi yeyote, kinyume chake ni tishio.

Katika ujumbe wake huo, Ghalibaf amesisitiza kuwa, “Marekani inamtoa kafara kila mtu kwa maslahi ya Israel, na wala haijali kumhusu yeyoye isipokuwa Israel.”

Spika wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa, Kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi ni tishio kwa nchi wenyeji wake, na wala hazikuanzishwa kwa ajili ya kuzilinda na kuzipa himaya nchi hizo.

Viongozi wa Iran wamesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitaki vita au uhasama na nchi za eneo, bali inalenga tu vituo vinavyotumiwa na Marekani kama chanzo cha mashambulizi dhidi ya ardhi yake.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, itaendeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4, ili kuwaadhibu vikali maadui walioanzisha uchokozi dhidi ya taifa hili mnamo Februari 28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *