Dar es Salaam. Kampuni ya kimataifa ya biashara ya mtandaoni, QNET, imejitokeza hadharani kuelezea msimamo wake kufuatia taarifa za hivi karibuni nchini Tanzania zinazohusisha madai ya utapeli unaodaiwa kufanywa na watu wanaojihusisha na jina la kampuni hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa mapema wiki hii jijini Accra, QNET imesema imepokea kwa masikitiko taarifa za kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kujihusisha na utapeli wa ajira wakitumia jina la kampuni hiyo, ikisisitiza kuwa haihusiki kwa namna yoyote na vitendo hivyo.

Kampuni hiyo imeeleza wazi kuwa haishirikiani na mtu au kikundi chochote kinachotumia jina lake kufanya shughuli zisizo halali, ikiwamo kuomba malipo ili kupata ajira, kutoa taarifa za kupotosha wakati wa usajili au kutumia shinikizo kuwashawishi watu kujiunga na biashara hiyo.

Aidha, QNET imefafanua kuwa haitoi ajira wala fursa za kusafiri nje ya nchi, bali mfumo wake unategemea Wasambazaji Huru (Independent Distributors – IDs) ambao ni wajasiriamali wanaojitegemea na kupata kipato kupitia mauzo ya bidhaa, si ajira ya kuajiriwa.

“Yeyote anayewahadaa wananchi kwa ahadi za ajira au kuomba fedha kwa kisingizio cha QNET anafanya udanganyifu na hana uhusiano rasmi na kampuni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha QNET imezipongeza mamlaka za Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na vitendo vya utapeli na imeahidi kuendelea kushirikiana nazo kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *