
Baada ya vita vya siku 40 vya muungano wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, utafiti wa kitaifa uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) umeonyesha kuendelea kusimama kidete kwa wananchi katika kuunga mkono vikosi vya ulinzi, mshikamano wa kitaifa na azma madhubuti ya kulinda uwezo wa nchi wa makombora na miundombinu ya kiulinzi.
Utafiti huo, uliowahusisha maelfu ya Wairani kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wakati na mara tu baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa, umeonyesha kuwa idadi kubwa ya washiriki wanaamini Iran haipaswi kukubali madai ya kupitiliza ya Marekani yanayolenga makubaliano ya kumaliza vita kikamilifu.
Wengi wa Wairani waliohojiwa wanaamini kuwa nchi inapaswa kukataa makubaliano yoyote yatakayoweka vikwazo kwa sekta ya makombora, kuhitaji kuondolewa kilo 400 za urani iliyorutubishwa au kulazimisha kusimamisha mchakato wa urutubishaji wa urani. Aidha wananchi waliowengi nchini Iran wanapinga makubaliano yoyote yatakayoruhusu meli zote kupita bila masharti katika Lango Bahari la Hormuz. Pia Wairani wanapinga makubaliano yatakayoilazimisha Iran iache kuunga mkono harakati za Muqawama au mapambano ya Kiislamu katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Swali kuu kwa washiriki lilikuwa kama Iran inapaswa kukubali au kukataa madai ya kupitiliza yaliyotolewa na Marekani kama masharti ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita. Majibu yalikuwa wazi:
Washiriki 85.7% walisema Iran haipaswi kukubali vikwazo kwa sekta ya makombora. Aidha 82.6% wamesema Iran isikubali kupelekwa nje ya nchi kwa kilo 400 za urani iliyorutubishwa. Halikadhalika washiriki 79.4% wamesema Iran haipaswi kukubali kusimamishwa urutubishaji urani ndani ya nchi, huku 73.7% wakisisitiza kuwa Iran isiafiki takwa la meli kupita bila masharti katika Lango-Bahari la Hormuz. Pia 68.1% wamesema Iran katu isikubali kukatisha ushirikiano na Mhimili wa Muqawama.
Wachambuzi wanasema matokeo hayo yanaonyesha “ukomavu wa kimkakati” katika jamii ya Iran, kufuatia vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.