Geita. Wawekezaji katika sekta ya viwanda pamoja na makandarasi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi, wameshauriwa kuthibitisha bidhaa zao na kupata nembo za ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua itakayoongeza thamani ya bidhaa na huduma zao katika masoko ya ndani na kimataifa.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 29, 2026 na Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene, wakati wa maonyesho ya makandarasi, wahandisi na watengenezaji wa mitambo ya uchimbaji madini yanayoendelea katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan vilivyopo Manispaa ya Geita.
Makene amesema uthibitishaji wa bidhaa ni hatua muhimu inayosaidia kuongeza uaminifu kwa walaji na hivyo kurahisisha upatikanaji wa masoko makubwa, ikiwemo ya kimataifa.
“Unapothibitisha bidhaa, unaiongezea thamani na kuifanya iwe rahisi kuuzika sokoni, ikiwa ni pamoja na kupenya katika masoko ya kimataifa kwa kuwa inakuwa imekidhi viwango vinavyoaminika,” amesema Makene.
Baadhi ya mitambo inayotumika kwenye shughuli za Madini na ujenzi, ni miongoni mwa mitambo iliyopo kwenye maonyesho ya wahandisi, wakandarasi na watengenezaji wa mitambo ya uchimbaji madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema katika jitihada za kurahisisha huduma kwa wawekezaji, TBS imefungua ofisi Kanda ya Ziwa Magharibi inayohudumia mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera, hatua iliyolenga kupunguza usumbufu wa kufuatilia vibali vya usajili wa bidhaa.
Kwa mujibu wa Makene, hadi sasa jumla ya vyeti 139 vya ubora vimetolewa huku vyeti 41 kati ya hivyo vikitolewa kwa wawekezaji wapya.
Aidha, amesema TBS ina jukumu la kukagua na kurasimisha huduma mbalimbali zikiwemo uhandisi wa mitambo, kemikali, vyakula, umeme, ujenzi, nguo pamoja na sekta ya madini na mazingira. Katika hilo, amewataka wakandarasi na wadau wengine kutumia viwango vya Tanzania badala ya kutegemea viwango vya nje.
Makene pia amesema maabara za shirika hilo zimethibitishwa kimataifa katika upimaji na uhakiki wa bidhaa kwa kuzingatia viwango vya ubora, jambo linaloimarisha zaidi uaminifu wa bidhaa zinazothibitishwa na TBS.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliotembelea maonyesho hayo wameiomba TBS kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kwa kuwafikia moja kwa moja katika maeneo yao badala ya kutegemea maonyesho pekee.
Mmoja wa wananchi hao, Anastazia John amesema kuna umuhimu wa elimu hiyo kuwa endelevu ili kuwasaidia watumiaji kutambua bidhaa zilizoidhinishwa.
Baadhi ya mitambo inayotumika kwenye shughuli za Madini na ujenzi, ni miongoni mwa mitambo iliyopo kwenye maonyesho ya wahandisi, wakandarasi na watengenezaji wa mitambo ya uchimbaji madini yanayoendelea mkoani Geita.
“Tunaomba elimu hii isiishie kwenye maonyesho tu, bali iwafikie wananchi mara kwa mara kwenye maeneo yetu, kwa kuwa kila siku kuna bidhaa mpya zinaingia sokoni,” amesema Anastazia.
Maonyesho hayo yalianza Aprili 24, 2026 na yanahusisha wakandarasi, wahandisi, watengenezaji wa mitambo ya uchimbaji madini pamoja na wajasiriamali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Geita. Yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 3, 2026, huku zaidi ya kampuni 40 za kimataifa zikishiriki.