Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imesema bado inatafakari pendekezo la Marekani la kumaliza vita vinavyoendelea, huku taarifa zikidai kuwa pande hizo mbili zinaweza kuwa karibu kufikia makubaliano mapya ya amani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Axios, Ikulu ya Marekani inaamini inaweza kufikia makubaliano ya vipengele 14 na Iran, ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa vikwazo na kurejeshwa kwa usafiri huru katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema Tehran bado inapitia pendekezo hilo na baadaye itawasilisha msimamo wake kupitia wapatanishi kutoka Pakistan.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Iran wameonyesha msimamo mkali, wakisema Marekani haitapata kupitia vita kile ambacho imeshindwa kupata kupitia mazungumzo ya moja kwa moja, huku wakionya kuwa Iran iko tayari kujibu mashambulizi yoyote mapya.
Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo ya saa 24 zilizopita yamekuwa mazuri na kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano, huku akisisitiza kuwa Iran haitaruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia.