Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi watakaopisha mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Masasi mkoani Mtwara hadi Mahumbika mkoani Lindi.
Akizungumza Mei 7, 2026 katika Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, ikiwemo ujenzi wa njia za kusafirisha umeme zitakazosaidia kuunganisha mikoa ya kusini kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema zaidi ya Sh5.1 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wapatao 1,730 katika mikoa ya Lindi na Mtwara watakaopisha mradi huo muhimu wa miundombinu ya nishati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange
Kwa mujibu wa Twange, awamu ya kwanza ya malipo itahusisha kaya 78 kutoka vijiji vya Kiwalala na Mahumbika, ambazo zitapatiwa zaidi ya Shilingi milioni 253 kabla ya zoezi hilo kuendelea katika maeneo mengine.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amesema ulipaji wa fidia unalenga kuhakikisha wananchi wote wanaoguswa na mradi huo wanalipwa stahiki zao kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuidhinisha zaidi ya Shilingi bilioni 5.1 kwa ajili ya fidia kwa wananchi zaidi ya 1,700 katika Lindi na Mtwara. Lengo ni kuhakikisha mradi huu wa Masasi hadi Mahumbika unatekelezwa kwa mafanikio,” amesema Mwanziva.
Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika vijiji 46 vilivyopo katika wilaya za Lindi, Ruangwa, Newala na Masasi, ambapo kwa kuanzia malipo yanaanza katika vijiji 14 vya Halmashauri ya Mtama.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika ukanda wa kusini mwa Tanzania, ambao kwa sasa unategemea zaidi umeme unaozalishwa kupitia gesi asilia mkoani Mtwara na kusafirishwa umbali mrefu.