Dar es Salaam. Wiki tatu zijazo nitakuwa mikoa ya Iringa na Njombe, kujaribu kukusanya nyimbo asili za watoto. Pamoja na nyimbo za watoto za Kiswahili kama vile, Ukuti, ukuti, wa mnazi wa mnazi au Seremala nipasulie mbao, walia kweche msumeno, pia nategemea kukusanya nyimbo za kiasili za Kihehe, Kibena, Kidzungwa na Kikinga.
Kibaridi cha Iringa kimenikumbusha bendi mbalimbali zilizowahi kuwapo katika mji huu. Hakika katika miaka ya nyuma mji ulichangamka sana kimuziki. Nikirudi nyuma sana kwenye miaka ya 1940, kwa taarifa iliyomo kwenye kipande cha gazeti cha mwaka 1947, Iringa tayari kulikuwako na bendi mbili Atomic Band na Wizard Band, na pia kulikuweko na kundi la muziki la wanawake lililokuwa likiitwa Salda na kundi hili lilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki mahiri wa wakati huo Bwana Abdul Pangamawe. Vikundi hivyo vilikuwa vikifanya maonyesho yao kwenye ukumbi wa Social Welfare.
Vikundi vingi vilifuata baada ya hapo kikiwamo kikundi cha Boni Band. Bendi hii pia ilikuwa na klabu ya mpira iliyoitwa kwa jina hilohilo. Hilo jina la Boni ambalo lilikuwa ni kifupi cha Born Town, lilikuwa na maana kubwa sana kihistoria.
Pamoja na mji wa Iringa kuitwa mji wa Wahehe, mji huu haukuanzishwa na Wahehe, mji ulianza kama kambi ya askari wa jeshi la Wajerumani mwaka 1896. Boma na makao makuu yalijengwa kilipo kituo kikuu cha polisi Iringa na jengo hilo bado liko.
Maofisa wachache wa Kijerumani waliokuwako walikuwa wakiishi mtaa unaoangaliana na soko kuu la Iringa.
Jirani na soko ni sehemu inayoitwa Miyomboni na hapo ndipo askari wa jeshi la Wajerumani, askari ambao walitoka makabila mbalimbali wengine wakiwa Wanubi, Wamanyema, Wanyamwezi na Wazaramo.
Na hawa ndio walikuwa wakazi wa kwanza wa mji huu, ulioitwa New Iringa, wakati Kalenga ambako ndiko kulikuwa na ikulu ya Wahehe kukiitwa Old Iringa. Kwa sababu hiyo, watoto na wajukuu wa wakazi hawa wa kwanza wa Iringa walikuwa wakijiita Boni. Timu ya mpira ya Boni iliendelea kuweko mpaka miaka ya 1960.
Bendi nyingine zilizokuwapo ni Habanero Band, mmoja wa wanamuziki alikuwa Bwana Nuhu Sapi aliyekuwa maarufu kwa jina la Anko.
Miaka ya 60, Bwana Abdu Pangamawe na wenzie wakawa na bendi maarufu sana iliyoitwa Highland Stars Band.
Bendi hii ilifanikiwa kurekodi nyimbo zake saba na hivyo kuacha kumbukumbu ya kudumu. Kati ya nyimbo walizorekodi zilikuwa, Kivinzi Nyerere, Yula Ngumwenda na Sita Sita mpenzi.
Kama zilivyokuwa bendi nyingine za awali, Highland Stars walikuwa wakiporomosha muziki wao katika ukumbi wa Social Welfare uliokuwa ukitumika miaka 1940, lakini serikali ya mkoloni ukauboresha zaidi na hata jina lika badilika na ukumbi ukawa maarufu kwa jina la Welfare Center. Wenyeji waliuita Olofea senda. Abdu Pangamawe ndie baba mzazi wa Ridhwani Pangamawe, mpiga solo mahili wa bendi ya Msondo.
Mkwawa High School nayo ikaja kuwa na bendi nzuri sana. Bendi hii iliyokuwa ya wanafunzi ilituimia ukumbi huo kuburudisha karibu kila Jumapili mchana. Bendi hiyo pia iliweza kurekodi katika studio za RTD. Baadhi ya nyimbo zao zikiwa Wikiendi Iringa, Eliza.
Bendi nyingine iliyofuata ilikuwa ndogo iliitwa Iringa Jazz Band lakini ilifahamika zaidi kwa jina la Chikwala chikwala. Bendi hii iliwahi pia kurekodi nyimbo zake katika studio za TFC, baadhi ya nyimbo zake zilitumika kwenye filamu iliyoitwa Wimbo wa Muanzi, filamu iliyokuwa inaongelea mradi wa kutumia mianzi kusambaza maji vijijini.
Pamoja na udogo wake baadhi ya wanamuziki wake walikuja kujiunga na bendi kubwa na kuweka alama katika historia ya muziki wa Tanzania. Mfano Ally Makunguru. Aliyekuja kung’ara katika bendi, za JKT Kimbunga, IOSS Ndekule, Mlimani Park, MK Group na baadaye kuhamia kwenye bendi za Kenya.
Hashim Kasanga aliyekuja kujiunga na TX Seleleka, kisha Tancut Almasi, Juma Msosi na Mamado Kanjanika waliokuja kuwa waanzilishi wa Tancut Almasi Orchestra, William Maselenge aliyewahi kuja kuwa mwanamuziki wa Orchestra Mambo Bado, Musoma Jazz Band, Maquis Original na hatimaye Tancut Almasi Orchestra, Ally Lashku aliyekuja kuwa mwanamuziki wa TX Seleleka na Watafiti Band na John Kitime aliyewahi kuwa mwanamuziki wa Orchestra Mambo Bado, Orchestra Makassy, Orchestra, TX Seleleka, Tancut Alamasi Orchestra, Vijana Jazz Band, Magoma Moto Sound na Kilimanjaro Band.
Katikati ya miaka ya 1980, wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga alamsi cha Iringa, Iringa Diamond Cutting Company, walichanga fedha na kununua vyombo vya bendi na ndipo ikazaliwa bendi kubwa zilizowahi kutoka Iringa Tancut Almasi Orchestra.
Bendi hii iliyokuwa na wanamuziki kutoka Tanzania na Kongo ilitikisa nchi nzima kwa nyimbo zake nyingi kupitia mitindo yao kama Mangala dance, Fimbo lugoda na Mbuguswa. Mambo yataendelea….