Tanga. Andrea Chambo ni baba mzazi wa Abdallah Chambo, mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ambaye aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana Mei 5, 2026 katika Mtaa wa Kilole, Kata ya Chanika, Tarafa ya Chanika, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Baba huyo anasema mwanawe, licha ya kufanya biashara ya kawaida ya bodaboda, alikuwa tegemeo kubwa nyumbani kwao na mchango wake kwa familia ulikuwa wa msingi katika maisha ya kila siku.

Andrea anasema anamkumbuka mwanawe huyo wa kwanza katika familia kwa mambo mengi mazuri kutokana na sifa yake ya upole, hekima na busara. Anaeleza kuwa Abdallah alikuwa mtoto aliyependa amani na aliyeishi vizuri na kila mtu, hali iliyomfanya kupendwa na jamii iliyomzunguka na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengi.

Anasema taarifa za kutoweka kwa mwanawe zilianza majira ya saa moja na dakika 45 usiku, lakini baadaye zilipatikana taarifa kamili za tukio hilo. Familia iliamua kumficha kwanza kutokana na hofu ya namna angepokea taarifa hizo, lakini baadaye walimueleza ukweli wa kilichotokea, jambo lililomuumiza sana kutokana na ukaribu mkubwa aliokuwa nao na mwanawe.

“Mida ya saa nne ndipo taarifa zilifika kwa familia, lakini kwangu zilicheleweshwa kwa sababu waliamua kunisitiri kwanza,” anasema Chambo.

Anasema kwa sasa kuna taarifa nyingi zinazomfikia kuhusu mazingira ya mauaji ya mwanawe, lakini hawezi kuzizungumza hadharani kabla ya kuzichuja vizuri. Anaeleza kuwa bado ni mapema kumtaja mtu yeyote kuwa amehusika huku akisema anatazama pia mahusiano na marafiki wa karibu wa marehemu ili kuona kama kulikuwa na tofauti zozote zilizoweza kusababisha tukio hilo.

“Msiba huu ni mzito sana. Naomba vyombo vya uchunguzi viendelee kufanya kazi yake ili siku moja familia iweze kusikia watu waliohusika katika mauaji haya wametiwa nguvuni na kuchukuliwa hatua za kisheria. Hii iwe fundisho la kukomesha matukio ya aina hii,” anasema Chambo.

Chambo anasema maneno ya mwisho anayoyakumbuka kutoka kwa mwanawe yalihusu ndoto na maisha ya familia yake.

“Mara ya mwisho tulivyoonana alinieleza kuhusu familia yake. Alikuwa tayari ana watoto wawili, mmoja nje ya ndoa na mwingine kwa mwanamke aliyekuwa akiishi naye. Alikuwa na mipango ya kufunga ndoa rasmi, kuanza maisha mapya na kununua pikipiki yake mwenyewe kwa ajili ya biashara ya bodaboda. Hilo ndilo lilikuwa lengo lake kubwa,” anasema baba huyo.

Anasema Abdallah pia alikuwa na maono ya kujenga nyumba yake mwenyewe kwa kuwa alikuwa akiishi kwa baba yake mkubwa. Tayari alikuwa ameanza kutafuta kiwanja kwa ajili ya kutimiza ndoto hiyo. Chambo anatoa wito kwa vijana wanaofanya biashara ya bodaboda kushirikiana kubaini wateja wenye nia mbaya kabla ya kuwabeba.

“Kwa maelezo ninayopewa, watu waliotekeleza uhalifu huo walifika muda mrefu kwenye kituo cha bodaboda. Wenzake walikuwa tayari wamewatilia shaka na wakakataa kuwabeba. Mwanangu alipofika hakujua yote yaliyokuwa yameendelea, akawachukua ndipo yaliyotokea yakatokea,” anasema Chambo.

Anaongeza kuwa bado anaumia moyoni akifikiria kuwa huenda kama wenzake wangempa tahadhari mapema, maisha ya mwanawe yangeokolewa.

“Wangemwambia mapema kuwa waliwatilia shaka wale watu, huenda mwanangu asingechinjwa. Hilo linaniumiza. Sikuwahi kufikiri siku moja jambo la kutisha kama hili lingemtokea mwanangu,” anasema.

Anasema jamii imeguswa na kifo hicho, jambo lililoonekana kupitia idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mazishi yake.

“Familia itaendelea kumkumbuka kupitia watoto wake wawili aliowaacha. Nikiwaona hao watoto nitakuwa namwona mwanangu,” anasema baba huyo.

Bodaboda wenzake wa karibu pia wameeleza majonzi yao kufuatia tukio hilo.

Khalifa Ally anasema marehemu alikuwa kijana waliyekulia naye mtaani. Wakati yeye na wenzake wanaanza kazi ya bodaboda, Abdallah alikuwa bado anaendelea na masomo. Baada ya kuhitimu, aliungana nao kufanya kazi hiyo huku akionyesha nidhamu na upendo mkubwa kwa watu wote waliomzunguka.

“Marehemu alikuwa na kazi mbili alizozipenda sana. Alikuwa anapenda muziki, hasa kazi za DJ, huku akiendelea na biashara ya bodaboda. Kuna kipindi alisimama kidogo kufanya bodaboda na kwenda kujifunza kazi hiyo ya muziki ambayo pia ilikuwa chanzo chake cha mapato hadi umauti ulipomkuta,” anasema Ally.

Anaeleza kuwa Abdallah alikuwa mtu wa kazi na aliyepambana kutafuta maisha kwa njia halali.

“Alikuwa anafanya yote. Wakati mwingine anafanya bodaboda, wakati mwingine anaitwa kwenye shughuli za muziki kwenda kufanya kazi yake ya DJ,” anaongeza Ally.

Ally anasema yeye na wenzake waliingiwa na mashaka mapema kutokana na tabia ya watu waliokuwa wanahitaji usafiri siku hiyo. Anaeleza kuwa watu hao walikaa kwa muda mrefu karibu na kibanda cha chipsi kilichokuwa kimefungwa katika eneo lenye giza huku wakijadiliana mambo yao kwa sauti za chini.

“Tulishawatilia shaka wale watu na tukawakataa. Mwenzetu alipokuja alisema, ‘Ngoja niombe Mungu,’ kisha akaondoka nao. Alipochukua muda mrefu kurudi tukaanza kupata hofu,” anasema Ally.

Anasema walipojaribu kumpigia simu, simu ndogo haikupatikana tena huku simu nyingine ikiita bila kupokewa. Hali hiyo iliwafanya waanze kumtafuta kwa kugawana makundi na kupitia maeneo mbalimbali waliyoelekezwa kuwa ndiyo walikokuwa wameenda.

“Tulipoenda kufuatilia ndipo tulimkuta marehemu akiwa amechinjwa, huku watu hao wakiwa wameondoka na pikipiki yake,” anasema.

Ally anasema tukio hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo, lakini la kwanza la namna hiyo.

“Kuna tukio lingine lilitokea ambapo bodaboda alipigwa na kujeruhiwa vibaya kisha pikipiki yake kuibiwa. Lakini hili la mtu kuchinjwa ni tukio la kwanza la aina yake hapa Handeni,” anasema.

Anasema mazingira waliyoikuta miili yalikuwa ya kutisha.

“Walikuwa wamemshika na kumchinja kisha wakamuacha akiwa amelala pale, kichwa chake kikiwa karibu kujitenga na kiwiliwili. Ni tukio ambalo limetuumiza,” anasimulia.

“Watu hao sijawahi kuwaona popote. Walitaka kubebwa na bodaboda yoyote lakini wengi walikataa baada ya kuwatilia shaka. Kijana huyo enzi za uhai wake, alipofika akawachukua na walipoelekea upande wa ofisi za madini ndipo walimwingiza kwenye kichochoro na kumchinja,” anasema.

Anaongeza kuwa haiwezi kusemwa moja kwa moja kwamba watu hao walikuwa wakimlenga marehemu binafsi kwa sababu siku hiyo alikuwa ametumia pikipiki ya ndugu yake.

“Alikuwa amepewa pikipiki kwa ajili ya kupeleka watu msibani. Aliporudi alikuwa amenyeshewa mvua, akaenda kubadilisha nguo nyumbani. Aliporudi maskani ndipo akawakuta wale watu na kuondoka nao,” anasema.

Katibu wa Bodaboda Wilaya ya Handeni, Khamis Kidunda maarufu kwa jina la Sakatonge, amesema tukio hilo limewashtua waendesha bodaboda wilayani humo.

Anasema matukio mengi ya uhalifu dhidi ya waendesha bodaboda hutokea nyakati za usiku huku wahalifu wakitumia mbinu ya kusafiri wawili wawili ili kutekeleza uhalifu wao kwa urahisi.

“Tunaviomba vyombo vya uchunguzi viharakishe uchunguzi ili waliofanya ukatili huu wakamatwe. Waendesha bodaboda wanahitaji elimu zaidi kuhusu namna ya kutambua abiria wenye nia ovu,” anasema Sakatonge.

Anasema ni vigumu mtu mmoja kutekeleza mauaji ya namna hiyo bila kusaidiwa na mwingine, hali inayowafanya wahalifu wengi kutumia mbinu ya kuwa wawili.

“Changamoto kubwa kwa bodaboda ni matukio ya uporaji, kujeruhiwa na kuuawa. Tukitoa elimu vizuri tunaweza kupunguza matukio haya yanayotokea hasa nyakati za usiku,” anasema.

Anashauri waendesha bodaboda kuanza kuwahoji abiria wanaowachukua usiku ili kubaini usalama wao kabla ya safari.

“Ukikutana na abiria usiku muulize anakwenda kwa nani, anamfahamu nani kule anakoenda. Ukiona anaanza kuyumba kwenye majibu, hapo ujue kuna tatizo,” anasema.

Anaongeza kuwa baadhi ya abiria hukasirishwa na maswali hayo, jambo linalowafanya baadhi ya madereva kuwaogopa ili wasikose kipato.

“Abiria wengine wanakwambia, ‘Unanipeleka au hunipeleki?’ Hapo utakuta bodaboda mwingine anamchukua kwa sababu tangu asubuhi hajapata mteja. Lakini lazima tuwe makini,” anasisitiza.

Sakatonge anasema ni muhimu kwa madereva wa bodaboda kuanza utamaduni wa kuomba vitambulisho au hata kupiga picha za abiria wanaowabeba usiku kwa ajili ya usalama wao.

“Ukiona mtu haeleweki, ni bora hata kwenda naye moja kwa moja kituo cha polisi kuliko kuhatarisha maisha yako,” anasema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku likiomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuwabaini waliohusika na mauaji hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *