Dar es Salaam. Kwa Miaka zaidi ya kumi sasa, Maua Sama, 35, ameendelea kujitambulisha kama mwanamuziki mwenye uwezo mkubwa wa kuimba miondoko ya RnB na Afropop huku mvuto wa sauti yake ukimbeba.
Maua, mkali wa kibao cha Niteke (2019), ni miongoni mwa wasanii wachache wa kike kutokea kwenye Bongofleva ambao wamefanikiwa kuwa na mwendelezo mzuri wa kazi zao katika miaka hii 10.
Kwa mujibu wa Maua, mastaa kama Ray C na Lady Jaydee, ndio hasa waliomvutia hadi kuamini na yeye siku moja anaweza kuja kuwa mwimbaji mkubwa na maarufu kama wao, ndoto ambayo tayari imetimia.
Hata hivyo, safari ya Maua kimuziki hadi kuja kufikia kilele cha mafanikio yake, imehusisha watu wengi wakiwamo wasanii wenzake ambao kupitia ushirikiano wao alipiga hatua na kuweka rekodi ya kipekee.
Miongoni mwa wasanii hao ni Mwana FA (Hamis Mwinjuma) ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na wengine ni Hanstone na Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music.
1. Mwana FA
Umaarufu wa Maua Sama kimuziki ulikuja baada ya kuachia wimbo wake aliomshirikisha Mwana FA, So Crazy (2013) ambao ulitayarishwa na Marco Chali katika studio za MJ Records, zamani MJ Production.
Hata hivyo, kabla kurekodi na Mwana FA, rapa aliyetoka na ngoma yake, Ingekuwa Vipi (2002), Maua aliwatumia wimbo huo wasanii kadhaa akiwamo Alikiba, Ommy Dimpoz na Ben Pol ili ashirikiane nao ila hakufanikiwa.
Tayari alikuwa amerekodi wimbo huo akiwa kwao Moshi na wakati huo alikuwa bado mwanafunzi. Mwana FA alipousikia akaamua urudiwe kurekodiwa, na ulipotoka tu ukamtambulisha vizuri Maua akitajwa kama mmoja wa waimbaji wakali.
Baada ya Maua kuvuma na wimbo huo (So Crazy), alijiunga na Tanzania House of Talent (THT) ili kujifunza zaidi muziki na ndipo hapo akaibuka na wimbo wake, Mahaba Niue (2016) uliompaisha zaidi.
Kwa mujibu wa Maua, baada ya kumaliza kurekodi wimbo huo pale THT kwa Emma the Boy, January Makamba na Babu Tale waliupenda sana na kupendekeza utoke kwa haraka, na kweli ulipotoka ukamleta Maua mwingine wa Afropop.
Alipata jina kubwa kimuziki, Maua aliendelea kuwa na ukaribu wa kikazi na Mwana FA ambaye amemshirikisha katika nyimbo zake tatu, Hata Sielewi (2017), Gwiji (2020) na Sio Kwa Ubaya Remix (2022) ambao toleo la awali alisikika Harmonize.
2. Hanstone
Tangu ameanza muziki, hakuna wimbo wa Maua wenye mafanikio makubwa katika majukwaa ya kidijitali (digital streaming) kama Iokote (2018) ambao alimshirikisha Hanstone, mtoto wa mwanamuziki wa zamani Banza Stone.
Mathalani video yake imeshatazamwa (views) YouTube zaidi ya mara milioni 34, huku video yake inayofuatia (Nitampata Wapi) ikiwa na milioni 5, hivyo ni Iokote ngoma kubwa zaidi kwake ukilinganisha na nyingine.
Iokote ni wimbo ambao haukuwa katika mipango yake mikubwa kwa mwaka huo. Wimbo uliokuwa katika mipango yake ni Amen (2018) akishirikiana na Ben Pol, ila Iokote ulipotoka muda mfupi baadaye ukafanya vizuri na kumpatia show nyingi.
Kulingana na Maua alishauriwa asimuweke Hanstone katika wimbo huo (Iokote) kutokana hakuwa msanii mkubwa wakati huo ila akasema ngoja ampe nafasi kama Mwana FA alivyomkubalia kolabo akiwa hajulikani.
Wimbo huo hakumpatia tu sifa nzuri Maua, bali na Hanstone ambaye wengi walimtazama kama mwanamuziki chipukizi anayekuja kwa kasi, hivyo akipewa nafasi atafika mbali.
Ndipo rekodi lebo ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz akamchukua na akaanza kurekodi nao lakini kabla ya kutambulisha makubaliano yao yakavunjika, kitu ambacho kinatajwa kumyumbisha.
3. Alikiba
Mara kadhaa Maua amekaririwa akisema kuwa kati ya waimbaji wa Bongofleva anaowapenda na kuwakubali sana, ni pamoja na Alikiba, mshindi wa tuzo ya MTV EMAs 2016 kama Msanii Bora Afrika.
Pengine hiyo ndio sababu kuu kwanini Maua aliamua kumshirikisha Alikiba katika nyimbo zake mbili ambazo zina maana kubwa katika historia ya muziki wake.
Tangu ametoka kimuziki mwaka 2013, Maua hajatoa albamu ila amefanikiwa kuachia Extended Playlist (EP) mbili, Cinema (2022) na Sama (2024), yenye nyimbo tano.
Alikiba ndiye mwanamuziki pekee ambaye ameshirikishwa katika EP zote mbili! Hatua hii inaonyesha ni kiasi gani Maua ana imani naye katika uwezo wake na ukubwa wa chapa yake.
Katika EP ya kwanza, Cinema (2022), Alikiba alisikika katika wimbo ‘Nioneshe’ ambao ulifanya vizuri, na katika EP ya pili, Sama (2024), Alikiba kashirikishwa katika wimbo ‘Itakuwaje’ ambao pia umepokelewa vizuri.
Cha kushangazwa ni kwamba video za kolabo hizo, zote hadi sasa zimetazamwa YouTube mara milioni 2.7, hivyo zimefungana kinamba, huku zikishika nafasi ya tatu katika orodha ya nyimbo zake zilizofanya vizuri zaidi katika mtandao huo.