Kibaha. Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John (Niki wa Pili) amevunja ukimya kuhusu sintofahamu ya mgogoro wa ardhi katika eneo la Lupaso, Mtaa wa Vikawe uliosababisha mapigano kati ya wakazi na watu waliotajwa kama mabaunsa.
Mapigano hayo yaliyotokea alfajiri ya kuamkia Mei 6, 2026 yamesababisha vifo vinne, vitatu vikitokea papo hapo na kimoja, majeruhi aliyefia hospitalini siku mbili baadaye. Mbali na vifo, pia vurugu hizo zimesababisha majeruhi na uharibifu wa mali.
Akizungumzia mgogoro uliopelekea vurugu hizo, Niki wa Pili amesema umesababishwa na uvamizi wa ardhi.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
“Hadi zinatokea vurugu kulikuwa na hatua ya maridhiano, lakini wamiliki ambao ni ndugu wa familia ya Ngololo (Juma) na wavamizi walishindwa kufikia muafaka. Hadi tunakwenda kwenye maridhiano kulikuwa kuna ugumu hata yeye (mmiliki) kulifikia eneo lake.
“Nafikiri huyo mmiliki (Ngololo), baada ya hali hiyo, naye akaamua atumie nguvu kuwaondoa wavamizi ambao nao waliingia kwa nguvu. Naye (Ngololo) akaamua kujichukulia sheria mkononi, jambo ambalo si sahihi,” amesema.
Amesema hilo tukio linachunguzwa na polisi na upelelezi ukikamilika litafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo waliiambia Mwananchi kwamba mmiliki alipeleka mabaunsa waliokuwa na mapanga, nyundo na visu na kuanza kubomoa nyumba zilizokuwa kwenye eneo la Lupaso, hali iliyosababisha wananchi wa eneo hilo kupiga filimbi kuomba msaada kwamba wamevamiwa na kusababisha vurugu kubwa baina ya wakazi na mabaunsa.
Chimbuko la mgogoro
Akizungumza na Mwananchi jana Mei 8, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Niki wa Pili alieleza chimbuko la mgogoro huo kuwa ni uvamizi wa ardhi na kubainisha kwamba katika eneo hilo kuna viwanja 121 vya watumishi ambao hakutaja ni watumishi wa wapi. Vilevile kuna eneo la familia ya Ngololo ambavyo vyote vimevamiwa.
Amesema watumishi hao 121 na familia ya Ngololo ni wamiliki halali wenye hati kwani maeneo yao yalipimwa.
“Viwanja hivyo vilivamiwa, baadhi ya watu wakajenga,” amesema Mkuu wa Wilaya na kuongeza kuwa wananchi waliojenga walidai waliuziwa kati ya mwaka 2008 hadi 2019 mpaka mwaka 2023. Lakini baada ya kutokea kwa wamiliki halali, walikubali walitapeliwa awali walipovinunua na kuamua kufanya maridhiano na wenye maeneo ambao walikubaliana wayalipie upya kwa wamiliki Sh3,000 kwa kila mita moja ya mraba.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Akigusia hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vikawe, Shaban Ally Shaban amesema mwaka 2010, hata kabla ya yeye kuwa mwenyekiti, alikuta wananchi wanaishi bila migogoro ya ardhi hadi Februari 2025 ndipo ikaonekana waliuziwa maeneo ya watu.
“Wananchi ambao waliuziwa maeneo hapo walikubali wametapeliwa na kutaka maridhiano ambayo yaliongozwa na Mkuu wa Wilaya na pande zote mbili kuridhia na kuamua eneo lote lipimwe ili waliojenga wawalipe wamiliki.
“Huo ndio muafaka uliofikiwa na pande zote mbili kuuridhia. Walikuja wapima wakapima. Baada ya zoezi hilo wananchi wakiwa wanasubiri control number ili walipie ndipo wakasikia Ngololo amekataa maridhiano.
“Wananchi waliomba kikao na Mkuu wa Wilaya ambacho kilikuwa kifanyike Mei 6, 2026, lakini alfajiri ya kuamkia siku hiyo mmiliki alileta mabaunsa kama 300 wakiwa kwenye mabasi madogo sita aina ya Toyota Coaster na kuanza kubomoa nyumba na kusababisha vurugu kubwa,” amesema Mwenyekiti wa mtaa.
Kuhusu maridhiano, Mkuu wa Wilaya amekiri yalifanyika kati ya wavamizi na watumishi 121 wenye umiliki halali wa eneo hilo, lakini katika hayo maridhiano familia ya Ngololo ilikataa.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
“Wamiliki 121 waliridhia wavamizi wawalipe Sh3,500 kwa kila square meter moja na hilo limefanyika kisheria na wana mwanasheria wao,” amesema.
Amesema katika eneo ambalo vurugu zilianzia, Lupaso, maridhiano yalishindikana akibainisha kwamba hilo ni eneo la familia ya Ngololo.
“Ni watu watano wa familia moja ambao wana viwanja eneo hilo wamegawana. Dada yao yupo Marekani alikataa maridhiano na kutaka wakamalizane mahakamani. Ni eneo linajulikana kama Kwa Masista,” amesema.
Amesema katika eneo hilo wavamizi walikuwa wakitumia nguvu na kusababisha hata wamiliki kutoweza kuingia kwenye maeneo yao kutokana na usalama wao kuwa mdogo.
Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
“Tulifanya mikutano ya maridhiano. Changamoto ikawa wamiliki, matakwa yao yalikuwa ni yale maeneo yenye nyumba ndiyo wavamizi wayalipie na vile viwanja ambavyo havijajengwa wamiliki wachukue maeneo yao, kitu ambacho wavamizi hawakukubaliana nacho.”
Amesema changamoto nyingine ilikuwa kwa wavamizi ambao hawakutaka kutambua mipaka licha ya kwamba maeneo yote yalikuwa yamepimwa na wengine kuingia kwenye kiwanja kimoja na kingine nusu.
“Maridhiano yalishindwa kupata muafaka. Wavamizi wanataka walipie maeneo yote na wenye maeneo wanasema angalau wavamizi waliokwishajenga ndiyo walipie na maeneo mengine ambayo wavamizi hawajajenga warudishiwe.
“Mwisho wale wamiliki 121 waliamua kuridhia kuachia maeneo yao isipokuwa familia ya Ngololo. Tulipokosa muafaka tukakubaliana na kushauri basi waende mahakamani,” amesema.
Kuhusu vurugu zilizoibuka, Mkuu wa Wilaya amesema huo ni uhalifu ambao unapaswa kushughulikiwa kisheria na kusisitiza wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi.
“Kama kuna mtu amevamia eneo lako basi umtoe kwa sheria na taratibu na vilevile kuvamia eneo la mtu huko nako ni kujichukulia sheria mkononi,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Ameshauri pia mahali penye migogoro ya namna hiyo kama ilivyo eneo la Lupaso, inapotokea nafasi ya maridhiano pande zote mbili ziweke dhamira ya kuridhiana ili kupata muafaka.
“Mfano katika hili suala, wakati tuko kwenye maridhiano, upande wa wavamizi walikuwa wanaweka masharti mengi kwa mwenye mali na mwenye mali akaona masharti hayana faida ndiyo sababu tulikosa muafaka,” amesema.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na Ngololo amekamatwa kwa mahojiano zaidi na yupo mahabusu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase licha ya kutomtaja jina mmiliki wa eneo, aliiambia Mwananchi kwamba tayari amekamatwa kwa mahojiano.
Amesema majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa Tumbi na mmoja kati ya majeruhi wawili ambao hali zao zilikuwa mbaya hawaongei. Aliyemtaja kwa jina moja la Nassoro alifariki Mei 8, 2026 hivyo kufanya vifo kufikia vinne hadi leo Mei 9, 2026 saa 4:30 asubuhi.