
Uchunguzi mpya wa maoni unaonyesha kuwa asilimia 66 Wamarekani wanaamini kuwa Rais Donald Trump ameshindwa kutoa hoja iliyo wazi kuhusu vita vya kichokozi vya na Marekani na Israel dhidi ya Iran. Aidha Wamarekani waliwengi wanasema wamekumbwa na hali ngumu ya kifedha kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta baada ya mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Reuters/Ipsos uliotolewa Jumatatu, karibu asilimia 66 ya waliohojiwa walisema Trump hajawahi “kufafanua kwa uwazi” malengo ya kijeshi ya Marekani nchini Iran, na asilimia 63 walisema ongezeko kali la bei ya mafuta limeathiri hali yao ya kifedha.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa asilimia 65 ya walioshiriki wanalaumu Chama cha Republican kwa kupanda kwa bei ya mafuta, huku asilimia 27 wakilaumu chama cha Democrat.
Aidha utafiti wa Reuters/Ipsos mwishoni mwa Aprili uliweka kiwango cha uungwaji mkono kwa Trump katika asilimia 34, kiwango cha chini zaidi katika muhula wake wa pili.
Taarifa hizi zinakuja wakati wastani wa kitaifa wa bei ya galoni moja ya petroli ya kawaida kufikia Mei 11 nchini Marekani ni dola 4.52, huku gharama ikizidi dola 6.15 katika jimbo la California.
Bei ya mafuta ghafi ya petroli duniani ilipanda katika masoko siku ya Jumanne, huku wasiwasi juu ya makubaliano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuathiri matarajio ya upatikanaji wa nishati duniani.
Masoko yaliendelea kufuatilia kwa makini mvutano unaohusiana na Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya Trump kukataa pendekezo la amani lililotumwa hivi karibuni na Iran.