
Nyota wa timu ya soka ya Barçelona, Lamine Yamal, alimeonyesha kitendo cha kupigiwa mfano kwa kupeperusha bendera ya Palestina wakati wa sherehe ya ubingwa wa timu hiyo kama ishara ya kuwaunga mkono watu wanaokandamizwa wa Palestina.
Mojawapo ya picha zenye utata zaidi za gwaride la ubingwa la timu ya mpira wa miguu ya Barcelona ilikuwa ya Lamine Yamal akiwa kwenye basi la wazi, akipeperusha bendera ya Palestina. Tukio hilo limesambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha hisia tofauti miongoni mwa mashabiki wa soka na hata kwenye duru za kisiasa.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa eneo hilo, sherehe ya ubingwa wa ligi ya klabu ya Barcelona ilikusanya zaidi ya watu 750,000 katika mitaani ya Barcelona.
Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo ni mwanasiasa wa Uhispania, Gabriel Ruffian, ambaye amesifu kitendo cha mchezaji huyo wa soka wa kimataifa wa mpira wa miguu.
El Mundo imeripoti kuwa, si kawaida kwa wanasoka wa Uhispania, hasa vijana, kuchukua msimamo wa kisiasa kuhusu masuala nyeti kama vile kadhia ya Palestina, na kwa sababu hii, hatua ya ujasiri ya Yamal imepewa mazingatio makubwa.
Hatua ya Yamal ya kupeperusha bendera ya Palestina katika sherehe ya ubingwa wa timu ya Barcelona inaweza kufasiriwa katika fremu ya maoni ya umma wa Uhispania kuhusu suala la haki za Palestina na vita na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.