
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni muendelezo wa makali ya bei ya mafuta kung’ata mifuko ya Watanzania baada ya bei za bidhaa muhimu kuendelea kupanda kila siku.
Baada ya gesi ya kupikia, sasa ni saruji. Wanaotarajia au kuendelea kujenga nyumba na miradi mbalimbali ya maendeleo sasa watalazimika kuongeza kati ya Sh700 hadi Sh1,000 katika kila mfuko mmoja wa saruji wanaonunua, na kuendelea kulingana na umbali alipo.
Ongezeko la bei lililothibitishwa na wazalishaji wa bidhaa hiyo linatajwa kuchangiwa na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji zilizochochewa na kupanda kwa bei za mafuta.
Hayo yanafanyika wakati ambao Serikali imeweka ruzuku ya Sh259 kwa kila lita moja ya dizeli ili kupunguza makali ya bei kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kijamii, zikiwamo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma.
Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazoshuhudia athari hasi kupitia ongezeko la bei za mafuta, kufuatia vita inayoendelea Mashariki ya Kati, ambayo imesababisha mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafishaji wa mafuta, ikiwemo visima vya uzalishaji, maghala ya kuhifadhi na viwanda vya kusafisha mafuta, na hivyo kuathiri uwezo wa uzalishaji.
Wazalishaji
Kampuni ya Dangote Cement ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutangaza ongezeko hilo la bei kupitia taarifa yao kwa umma waliyoitoa Mei 11, 2026, ambayo iliweka wazi ongezeko la Sh700 kwa aina zote za saruji wanazozalisha.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko, Aggrey Masaoe, inaeleza kuwa kupanda kwa bei hizo kunatokana na kukua kwa gharama za usafirishaji.
“Kutokana na kuendelea kupanda kwa gharama za usafirishaji, pembejeo na gharama za uendeshaji kwa ujumla, Dangote Cement Limited Tanzania (DCLT) itafanya marekebisho ya bei za saruji zake kuanzia tarehe 12 Mei 2026, saa 00:00. Bei za aina zote za saruji, ikiwemo 32.5R, 32.5N, 42.5N, 42.5R na 52.5N, itaongezwa kwa Sh700 kwa kila mfuko wa kilo 50 (bila VAT) katika masoko yote,” imeeleza taarifa hiyo.
Wakati Dangote wakisema hayo, baadhi ya maofisa waliozungumza na Mwananchi kutoka kiwanda cha Mbeya Cement na JK White Cement nao wamekiri kuwapo kwa ongezeko hilo.
Akitaka asiandikwe jina kwa sababu taarifa hiyo inapaswa kutolewa kwa ruhusa ya uongozi, ofisa kutoka kiwanda cha saruji Mbeya, kinachohudumia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, alikiri kuwapo kwa ongezeko la Sh1,000 kwa mfuko wanaozalisha.
“Ni kweli bei imeongezeka tangu Mei 7, mwaka huu. Hii imetokana na ongezeko la bei ya mafuta iliyopandisha gharama za usafirishaji. Hali hii ndiyo iliyochochea mawakala wetu kupandisha bei,” amesema.
Kutoka JK White Cement, waliopo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, pia walikiri ongezeko la kuanzia Sh1,000 ambalo huongezeka kutokana na eneo ambalo mteja anachukulia.
“Ni kweli bei zimeongezeka, kuanzia Sh1,000, lakini hii sasa inategemeana na mazingira ambayo mtu yupo ili kushuhudia hali hii. Umbali alipo hadi mzigo unamfikia pia ndiyo utaonesha ongezeko hilo. Hii ni kwa sababu pia gharama za usafirishaji zimeongezeka,” amesema mtu huyo.
Nyati Cement nao wamekiri kuwapo kwa mabadiliko ya bei, licha ya kutotaja kwa kiwango gani, huku Twiga Cement na Tanga Cement nao wakikiri kuwapo kwa ongezeko hilo.
Tayari ongezeko hilo la bei limeshafika mtaani, na Sh1,000 imeongezwa katika kila mfuko. Mmoja wa wauzaji katika eneo la Madale jijini hapa amesema mfuko mmoja wa saruji aina ya Twiga Plus sasa ni Sh19,000 kutoka Sh17,500, huku ile iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh16,500 ikiuzwa Sh18,000.
“Bei zimepanda dada, tangu juzi huko kiwandani, hivyo sisi tunatafuta faida ndogo katika biashara hii,” amesema Massawe Masha, muuzaji wa duka hilo la vifaa vya ujenzi.
Kauli yake inaungwa mkono na Yusuph Maina ambaye amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la Sh1,500 kwa kila mfuko wa saruji.
“Bila kujali kampuni, na hiyo ni kwa sababu wanatuletea hadi hapa dukani. Tungekuwa tunafuata sisi, bei ingekuwa zaidi ya hiyo. Hivyo kwa mfuko uliokuwa ukiuzwa Sh16,500 sasa ni Sh18,000, kwa ule wa Sh17,500 sasa ni Sh19,000. Bei zinatofautiana kati ya kampuni,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa uchumi na Biashara, Dk Goodhope Mkaro, amesema suala hilo linaweza kufanya sekta ya ujenzi iwe na mdororo kwa kiasi tofauti na wakati ambao bei haikupanda.
Hiyo ni kwa sababu itapunguza uwezo wa watu kununua bidhaa, huku akieleza kuwa kama walikuwa wanapata mifuko 10 kwa Sh200,000, sasa itakuwa pungufu.
“Kinachoweza kuwasaidia kwa sasa ni kuwa na vipaumbele kwa kupunguza vitu ambavyo havina umuhimu ili waweze kuendelea na ujenzi,” amesema.
Amesema kuwekwa kwa ruzuku ya Sh259 kwa lita ya dizeli huenda ikawa imesaidia kwa kiasi kutokuwapo kwa ongezeko kubwa la bei, huku akisema kama isingekuwapo hali ingekuwa mbaya zaidi.
“Ushauri wangu kwa Serikali, vita ikiisha wahakikishe wanasimamia bei za bidhaa, ikiwemo saruji, zirudi katika bei zake za zamani, kwani mara zote bei zimekuwa zikipanda wakati kama huu, kushuka inakuwa ni ngumu,” amesema.