Nguvu ya wazazi yaondoa wanafunzi 300 sakafuni MakangaraweNguvu ya wazazi yaondoa wanafunzi 300 sakafuni Makangarawe

Dar es Salaam. Kilichokuwa kero ya muda mrefu kwa mamia ya wanafunzi waliolazimika kukaa chini madarasani katika shule za msingi Jitihada na Dovya, Kata ya  Makangarawe wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, sasa kimeanza kupata mwanga baada ya juhudi za pamoja za wazazi, viongozi na wadau wa elimu kuzaa matunda.

Mei 16, 2026, Diwani wa Makangarawe (CCM), Fadhili Mboga amekabidhi madawati 100 kwa shule hizo mbili, hatua iliyowaondoa angalau wanafunzi 300 waliokuwa wakisomea chini kutokana na uhaba mkubwa wa miundombinu ya kujifunzia.

Makabidhiano hayo ni matokeo ya ziara ya ukaguzi aliyoifanya Februari mwaka huu, Mboga alishuhudia msongamano na wanafunzi kukaa chini katika shule hizo zinazohudumia wanafunzi 4,600 kwa pamoja.

Hata hivyo, changamoto ya Makangarawe inaakisi hali inayojitokeza katika shule nyingi za msingi na sekondari nchini, bado kuna upungufu wa madawati, madarasa na vifaa vya kujifunzia kutokana na ongezeko la wanafunzi na uwepo mdogo wa miundombinu kwa baadhi ya shule nchini.

Wazazi wa wanafunzi shule za msingi Jitihada na Dovya, Makangarawe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, wakishiriki hafla ya kujadili changamoto za miundombinu ya elimu na kupokea madawati yaliyotokana na michango yao, Jumamosi Mei 16, 2026.

Katika muktadha huo, Serikali kupitia miongozo yake ya usimamizi wa sekta ya elimu imeendelea kusisitiza ushirikishwaji wa wananchi na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto za kijamii, hususan ngazi ya shule na halmashauri, sambamba na kuimarisha mipango ya ndani ya maeneo husika kuongeza rasilimali za elimu.

Katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba mapema mwaka huu mkoani Tanga, alibaini uhaba wa miundombinu ya elimu kwa shule nyingi yakiwamo madawati, madarasa na vitabu, hatua iliyomfanya kutoa maamuzi magumu katika baadhi ya maeneo na kuwataka watendaji wa halmashauri husika kusitisha posho na malipo ya huduma za ofisi zao na kuelekeza fedha hizo kwenye utatuzi wa changamoto hizo kwa haraka.

Mwelekeo huo wa ushirikiano wa jamii na Serikali, unaonekana pia katika hatua mbalimbali za halmashauri nchini; jamii inahamasishwa kushiriki katika kuboresha mazingira ya shule, badala ya kusubiri ufumbuzi kutoka ngazi za juu pekee.

Katika Kata ya Makangarawe, dhana hiyo imeanza kutafsiriwa kwa vitendo baada ya wazazi kuitikia wito wa kuchangia madawati kupitia mikutano ya pamoja ya kutafuta suluhisho la changamoto ya miundombinu hiyo iliyotokana na ziara ya diwani wa kata hiyo iliyobaini uhaba wa madawati na uchakavu wa miundombinu ya madarasa na vyoo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mboga amesema elimu ya msingi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya watoto na jamii kwa jumla, akiwataka wazazi kujitoa ili kuimarisha mazingira ya watoto wao kujifunza.

Diwani wa Makangarawe Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Fadhili Mboga, akizungumza na wananchi katika hafla ya kukabidhi madawati waliyochangia kukabili uhaba wa miundombinu hiyo kwa shule za msingi katani humo, Jumamosi, Mei 16, 2026.

“Mimi kama kiongozi wenu, jicho langu kwenye elimu ya msingi lipo katika shule hizi, Jitihada yenye wanafunzi 2,700 na Dovya yenye wanafunzi 1,900. Mimi katika utawala wangu nitasimama na taasisi hizi kama mdau wa kweli wa elimu,” amesema.

Amesema suluhisho la changamoto za elimu linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali za mitaa na wananchi wenyewe, wakati Serikali kuu ikiangazia changamoto za kitaifa ili kumaliza kero hizo.

“Shuleni ni nyumbani kwa wanafunzi, muda mwingi wanakuwa hapa kuliko nyumbani. Lazima tuweke mazingira rafiki kwao ili wasipachukie shule. Unakubali vipi mwanao akae chini kutwa nzima shule,” amehoji.

Amesema mafanikio ya madawati hayo yametokana na mwitikio wa wazazi baada ya kuombwa kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

“Nawashukuru wazazi wote ambao baada ya kuona changamoto ya madawati na baada ya kuwashirikisha wakawa tayari kuchangia. Kwa ushirikiano huu, ninaamini kila mzazi atakuwa na uchungu na madawati haya kwa kuwa tumeyatengeneza wenyewe,” amesema.

Diwani huyo pia amesisitiza uwekezaji katika michezo shuleni ili kuibua vipaji vya watoto wangali wadogo na kuchochea wanafunzi kupenda shule na kupunguza tatizo la utoro na wanafunzi kuacha shule.

Katika hatua hiyo, Mboga amekabidhi vifaa vya michezo ikiwamo mipira na sare za michezo kwa wanafunzi wa shule hizo ili kutekeleza kwa vitendo lengo hilo.

Ofisa Elimu wa Kata ya Makangarawe, Sofia Gyindo amesema  mwitikio wa jamii katika kuboresha mazingira ya elimu ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Diwani wa Kata ya Makangarawe, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Fadhili Mboga (wapili kushoto), akikabidhi vifaa vya michezo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Dovya, Jumamosi Mei 16, 2026. Wengine ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo (kulia) na Ofisa Elimu wa kata hiyo Sofia Gyindo.

“Tumekuwa na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule zetu, lakini hatua hii inaonesha kuwa ushirikiano wa jamii unaweza kuleta mabadiliko ya haraka,” amesema.

Akisoma taarifa ya michango ya wazazi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dovya, Salum Gawaza amesema jumla ya Sh1,033,500 imekusanywa kwa hiari ya wazazi kusaidia ununuzi wa madawati.

Amesema hatua hiyo imewaondoa wanafunzi 300 sakafuni na kuimarisha ushirikiano kati ya shule na jamii.

Mmoja wa wazazi walioshiriki, Janeth Jesephath amesema wazazi waliguswa na hali ya watoto wao na kuamua kuchukua hatua hiyo.

Amesema bado wanaendelea kutoa michango yao ili kuona tatizo hilo linaisha.

“Ilituuma kuona watoto wanakaa chini muda wote wa masomo. Tulipoona hali halisi, tuliona ni wajibu wetu kuchangia ili watoto wapate mazingira bora ya kujifunzia,” amesema.

Hatua ya Makangarawe inaonekana kama mfano wa dhana ya ushirikishwaji wa jamii katika sekta ya elimu, ikidokeza kuwa pamoja na changamoto ya kitaifa ya miundombinu, suluhisho linaweza kuanza kwa ngazi za chini ikiwa jamii itashirikiana na Serikali katika kuamua na kuchukua hatua za utatuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *