
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limesema mazungumzo ya hivi karibuni na maafisa wa soka wa Iran yalikuwa chanya na yenye kujenga, huku maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia la 2026 yakiendelea.
Kwa mujibu wa FIFA, Katibu Mkuu Mattias Grafström alifanya mkutano chanya na Mehdi Taj, rais wa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (FFIRI). Katika mkutano huo, pande zote mbili zilijadili masuala yanayohusiana na maandalizi na ushiriki wa Iran katika mashindano hayo makubwa ya soka duniani.
Grafström alieleza kuwa ana imani kuhusu ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia lijalo kufuatia mazungumzo hayo.
Akizungumza wakati wa ziara yake mjini Istanbul, Grafström alisema wamekuwa na mkutano mzuri pamoja na Shirikisho la Soka la Iran.
Hata hivyo, maswali zaidi yameibuka baada ya rais wa Shirikisho la Soka la Iran kunyimwa kuingia nchini Canada mapema mwezi huu ili kuhudhuria Kongamano la FIFA lililofanyika Vancouver. Hatua hiyo ilitokana na ukweli kwamba alikamilisha huduma yake ya kijeshi katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Nchini Iran, huduma ya kijeshi kwa muda wa miaka miwili ni ya lazima kwa wanaume wote baada ya kufikisha umri wa miaka 18. Mbali na jeshi la kawaida na polisi, wengi pia hutekeleza huduma hiyo ndani ya IRGC.
Marekani na Canada, ambazo kwa pamoja na Mexico ndizo wenyeji wa Kombe la Dunia la 2026, zimeiweka IRGC katika orodha wanayoitaja kuwa eti ya “makundi ya kigaidi”, hatua inayotazamwa kuwa na misukumo ya kisiasa. Nchi hizo pia zimeweka wazi kwamba hazitaruhusu kuingia kwa raia wa Iran waliowahi kutumikia huduma yao ya kijeshi ndani ya IRGC.
Iran imepangiwa kucheza mechi zake zote tatu za hatua ya makundi nchini Marekani. Hata hivyo, ushiriki wa timu hiyo katika mashindano yatakayofanyika kati ya tarehe 11 Juni hadi 19 Julai umekuwa ukizua mjadala, hasa baada ya mvutano wa kijeshi uliotokana na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Iran ilikuwa imeomba mechi zake za Kombe la Dunia zihamishwe kuchezwa nchini Mexico, lakini Rais wa FIFA Gianni Infantino amesisitiza kuwa mechi zote lazima zichezwe katika viwanja vilivyopangwa awali.
Timu ya taifa ya Iran inatarajiwa kuondoka Tehran siku ya Jumatatu kuelekea kambi ya mazoezi nchini Uturuki, kabla ya kuhamia kituo chake cha maandalizi nchini Marekani katika uwanja wa michezo wa Kino Sports Complex, mjini Tucson, Arizona, mapema mwezi Juni.
Iran imepangwa kuanza kampeni yake ya Kombe la Dunia kwa mechi dhidi ya New Zealand mjini Los Angeles tarehe 15 Juni. Baadaye itakutana pia na Ubelgiji na Misri katika Kundi G.
