Khadija Kopa alivyogeuka silaha kwa wasanii wa BongoflevaKhadija Kopa alivyogeuka silaha kwa wasanii wa Bongofleva

Dar es Salaam. Malkia  wa Taarabu nchini, Khadija Kopa amegeuka kuwa kipenzi cha wasanii wengi wa kizazi kipya (Bongofleva) jambo lililosababisha ashirikishwe zaidi kwenye nyimbo na kuwaacha mbali wakongwe wenzake.

Makala haya yanakuletea miongoni mwa vijana waliokoshwa na sauti ya malkia huyo ambaye alianza kazi ya sanaa mwaka 1990 katika kikundi cha Culture Musical Club, Zanzibar. 

1. Chid Benzi (2012)

Hakuna ubishi kuwa Chid Benzi ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo wa Bongofleva waliotambua kuwa sauti ya Khadija Kopa inauzika katika soko lao, hivyo akafanya kitu na kikasikika.

Wakaingia studio na kutengeneza wimbo, Nampenda Sana (2012). Hii ni kolabo nyingine ya Chid Benzi na msanii wa taarabu iliyofanya vizuri baada ya ile aliyofanya na Mzee Yussuf, Mashallah. Huyu alikuwa ni msanii mwingine mkubwa wa Hip Hop Bongo kufanya kolabo na nguli wa taarabu baada ya Fid Q aliyempa shavu Bi Kidude katika wimbo wake ‘Juhudi za Wasiojiweza’ kutoka katika albamu yake ya pili, Propaganda (2009).

Tayari Chidi ameshirikiana na wasanii wakubwa Bongo kama Alikiba, Diamond Platnumz, Ray C, Mwasiti, Marlaw, TID, Makamua, Tundaman, K-Lynn, Spack, Angeline, Lady Jaydee, Professor Jay, JCB, Mwana FA, Nako 2 Nako Soldiers, Young Dee, Mh. Temba n.k.

2. Diamond Platnumz (2015)

Kipindi Diamond ananza kuwika kimataifa ndipo alimshirikisha Khadija Kopa katika wimbo wake, Nasema Nawe (2015) ambao ulitayarishwa na Tudd Thomas aliyetengeneza ngoma nyingine kali za Diamond ikiwemo Utanipenda na Mdogo Mdogo.

Wimbo huo wenye mahadhi ya mduara ulifanya vizuri pia kimataifa, mathalan ulishika chati mbalimbali nchini Nigeria ambapo Diamond alivuna mashabiki kufuatia kolabo na Davido. Baada ya kolabo hiyo, Kopa aliwahi kueleza kuwa na mpango kuja kumshirikisha Diamond kufanya remix ya wimbo uitwao ‘Nipepee Mpenzi Wangu’ wa hayati mwanaye Omary Kopa aliyefariki mwaka 2007.

Diamond aliyetoka kimuziki mwaka 2009 na mwaka uliofuatia kushinda tuzo ya TMA kama Msanii Bora Chipukizi, tayari ametoa albamu tatu Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018) pamoja na EP moja, First of All (FOA) (2022). 

3. Aslay (2017)

Baada ya kuachana na Yamoto Band na kuanza kufanya kazi kama solo, Aslay alitoa wimbo, Usitie Doa (2017) na kumshirikisha Khadija Kopa ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kuachia kufuatia kuvunjika kundi hilo.

Wimbo huo ni moja ya nyimbo za Aslay zilizopata mapokezi makubwa ndani ya muda mfupi na hadi sasa video yake ikiwa na ‘views’ zaidi milioni 12 YouTube tangu itoke miaka sita iliyopita. Ikumbukwe wimbo wa kwanza Aslay kurekodi unaitwa ‘Niwe Nawe’ ambao alikuja kuurudia na kumshirikisha Mh Temba, ila ngoma iliyomtoa ni ‘Nakusemea’ ambayo ilibeba jina la albamu yake ya kwanza iliyotoka akiwa kidato cha pili.

Baadaye Aslay alikuja kuunda kundi la Yamoto Band pamoja wenzake watatu Beka Flavour, Enock Bella na Mbosso. Wote walikulia kimuziki katika kituo cha Mkubwa na Wanawe chake Mkubwa Fella, ila sasa kila mmoja anafanya kazi peke yake.

4. Zuchu (2020)

Huyu ni mtoto wa Khadija Kopa. Kama mama ameweza kufanya kolabo na wasanii wengine kwanini ishindikane kwa mwanaye? Basi wakaingia studio na kutoa wimbo ‘Mauzauza’ unaopatikana kwenye EP ya I Am Zuchu (2020).

EP hiyo ndiyo ilitambulisha Zuchu kimuziki baada ya kusainiwa WCB Wasafi kwa Diamond Platnumz na kwa ujumla ilishirikisha wasanii wawili tu, Khadija Kopa na Mbosso.

Hata hivyo, mambo hayakuishia hapo kwani baadaye Kopa alikuja kuonekana katika video ya wimbo wa Zuchu, Nani Remix (2023) akimshirikisha staa kutoka DR Congo, Innoss’b ambaye hapo awali alishafanya kazi na wasanii wa Tanzania, Diamond na Rayvanny.

Zuchu ni msanii wa pili wa kike kusainiwa WCB Wasafi baada ya Queen Darleen aliyesainiwa 2016 pamoja na Rich Mavoko, ila kwa sasa ni msanii wa pili wa lebo hiyo aliyefanikiwa zaidi kimuziki baada ya Diamond. 

5. Weusi (2021)

Hip Hop na taarabu zinakutana tena. Hapa kundi la Weusi linaoundwa na wasanii watano walipompa shavu Khadija Kopa katika wimbo wao ‘Penzi la Bando’ kutoka katika albamu ya kwanza, Air Weusi (2021) iliyotoka na nyimbo 14.

Kundi hilo linaloundwa na Joh Makini, G Nako, Lord Eyes, Bonta na Nikki wa Pili hiyo ndio ilikuwa kolabo kubwa zaidi katika albamu hiyo na video yake ilitoka ikiongozwa na Ivan, huku mwanamuziki Linah akitokea.

Na hadi sasa Weusi wamefanikiwa kutoa wimbo mmoja pekee ambao umekutanisha wasanii wote watano. Ngoma hiyo inaitwa ‘Watoto wa Mungu’ iliyotoka chini ya Bongo Records ya P-Funk Majani.

Ukiachana na hao, wasanii wengine wa Bongofleva waliowahi kufanya kazi na Khadija Kopa ni Bright, Bonge la Nyau na kadhalika, huku Kopa akisikika katika kolabo moja kali ‘Malkia wa Nguvu’ iliyowakutanisha Ray C, Linah, Nandy, Mwasiti na Maua Sama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *